Timu ya soka ya Tanzania, maarufu kama ‘Taifa Stars’ imekita kambi nchini Misri, ikijiwinda na Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2025, yaani AFCON 2025, itakayofanyika nchini Morocco.
‘Taifa Stars’, inayofundishwa na Muargentina Miguel Angel Gamondi, imekusanya jumla ya wachezaji 28, watakaopeperusha bendera ya Tanzania.
Tanzania, ambayo inashika nafasi ya 112 duniani na ya 27 kwa ubora wa soka barani Afrika, itakuwa ikitupa karata yake ya nne kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika, mara zote ikishindwa kuvuka hatua za makundi.
Katika michuano ya mwaka huu, ambayo itaanza kurindima Disemba 21, Tanzania ipo kwenye Kundi C, ikiwa na majirani zao Uganda, ma ‘Oga’ wa Nigeria na Watunisia.
Hakika itakuwa shughuli pevu kwa ‘Taifa Stars’ ambao watakuwa wakimtegemea mfungaji wao bora wa muda wote, Simon Msuva, pamoja na nahodha Mbwana Samatta, maarufu kama ‘Captain Diego’.
Disemba 23, Taifa Stars watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya mabingwa mara 3 wa AFCON, Nigeria iliyosheheni nyota kama vile Victor Osimhen, Ademola Lookman na mpwa wa Jay Jay Okocha, Alex Iwobi, ambaye anakiputa pale EPL akiwa na Fulham.
Siku nne baadaye, vijana wa Gamondi watakuwa wakipepetana na majirani zao Uganda; ile ya akina Khalid Aucho wa Singida Big Stars, kabla ya kukamilisha ratiba yao dhidi ya Tunisia, Disemba 30.
Ikumbukwe kuwa, hii ni michuano muhimu sana kwa timu ya taifa ya Tanzania, inapojiandaa na AFCON 2027, ambapo, wao, kwa pamoja na Kenya na Uganda, watakuwa wenyeji.
Mara ya kwanza kwa Tanzania kushiriki michuano ya AFCON ilikuwa ni mwaka 1980 nchini Nigeria, enzi za akina Jela Mtagwa, Leodgar Tenga, Peter Tino na wengine.
Kisha ikafuata mwaka 2019, na baadaye mwaka 2024, na kama nilivyosema hapo awali, ilishindwa kuvuka hatua za makundi.




















