MICHEZO
2 dk kusoma
Alphonse Simbu adakia dhahabu ya kwanza kabisa kwa Tanzania Katika Mashindano ya Dunia ya mbio-Tokyo
Hii ni medali ya kwanza ya dhahabu kwa Tanzania katika mashindano ya riadha ya dunia (au Olimpiki) katika mbio za marathon
Alphonse Simbu adakia dhahabu ya kwanza kabisa kwa Tanzania Katika Mashindano ya Dunia ya mbio-Tokyo
Hii ni dhahabu y akwanza kwa Tanzania katika mashindano ya mbio duniani/ Athletics Kenya / TRT Afrika Swahili
15 Septemba 2025

Mtifuo wa dakika za lala salama wa Alphonse Simbu ulifua dafu baada ya Mtanzania huyo kushinda mpinzani wa karibu zaidi kutoka ujerumani na kunyakua dhahabu.

Huu ni ushindi wa kwanza kabisa wa dhahabu kwa taifa hilo la Afrika mashariki lililozingirwa na mabingwa wa mbio za dunia.

Kiu cha kukwea kilele cha jukwaa hatimaye kilipozwa kufuatia ushindi huo wa Simbu wa saa mbili, dakika tisa na sekunde arobaini na nane (2:09.48)

Simbu, akishiriki katika mashindano yake ya tano ya riadha ya dunia, alikamu anguvu yake yote katika mojawapo ya mashindano magumu zaidi kuhimili hali ya joto kali iliyosababisha wanariadha 24 vigogo kujiondoa katikati, wakiwemo Waethiopia wote watatu; Tesfaye Deriba, Delesa Geleta, Tadese Takele, Mkenya Hillary Kipkoech na Waganda wawili; Stephen Kisa na Solomon Mutai.

Simbu, 33, ambaye alidumisha kasi yake katika sehemu bora zaidi ya mbio hizo, alimpokonya Mjerumani Amanal Petros ushindi kwenye kuvuka utepe na kumuachia fedha kwa saa 2:09:48 huku Mwitaliano Ilias Aouani akinyakua shaba kwa saa 2:09:53.

Mkenya Kennedy Kimutai alimaliza katika nafasi ya 16 kwa saa 2:11:45 huku mwenzake Vincent Kipkemoi akifanikiwa kuibuka wa 22, na kuwaacha Wakenya wakimezea mate taji hilo ambalo mwisho walinyakua 2017 mjini London kupitia Geoffrey Kirui. Wakati huo Simbu alimaliza wa tatu jukwaani.

Hii ni medali ya kwanza ya dhahabu kwa Tanzania katika Mashindano ya Riadha ya Dunia (au Olimpiki) katika mbio za marathon. Ni taji la kwanza kubwa la kimataifa la nchi hiyo katika mashindano haya.

Ushindi huo ulikuja katika mojawapo ya fainali zilizoleta uchangamfu mkubwa uwanjani wa kupishana kwa unyoya, jambo ambalo sio kawaida kwa mashindano ya masafa marefu. Hii inajulikana kama Photo finish, kwamba lazima wasimamizi wakague picha ili kubainisha mshindi.

Kwa Tanzania ubingwa katika kiwango hiki unaweza kuwatia moyo wanariadha wachanga, kupata usaidizi zaidi na uwekezaji wa mbio za masafa, na kuiweka Tanzania kwenye ramani zaidi katika utamaduni wa Afrika Mashariki wa mbio za marathoni.

Lakini kwa Simbu mwenyewe japo hapo awali alishinda shaba katika mbio za dunia 2017 na alikuwa na maonyesho ya nguvu (k.m. nafasi ya pili huko Boston mnamo 2025). Lakini dhahabu hii ni kilele - utambuzi wa miaka ya uvumilivu na maendeleo.

CHANZO:TRT Afrika Swahili