Kwa miongo kadhaa, kalenda ya uchumi nchini Zambia—na kwa hakika katika sehemu kubwa ya nchi zinazoendelea—ilifuata mzunguko unaotabirika na wa kuhuzunisha.
Msimu wa sikukuu, ambao kwa kawaida ni wakati wa shangwe na sherehe, ulikuwa ukifunikwa na hali ya udhaifu wa kiuchumi. Mahitaji ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na fedha za kigeni yalipoongezeka, sarafu ya kwacha ya Zambia ilikuwa ikizidi kudhoofika, jambo lililopunguza uwezo wa wananchi kununua na kuharibu hali ya furaha ya sikukuu.
Huu ulikuwa kama “ushuru wa msimu” wa kuyumba kwa uchumi, uliolipwa na kila raia. Hata hivyo, katika msimu wa sikukuu uliopita, jambo la kushangaza lilitokea. Kwacha haikubaki imara tu, bali pia ilizidi kuimarika—tukio la kihistoria lililovunja mtindo ambao wengi walikuwa wameukubali kama mienendo isiyobadilika.
Hili si tukio la bahati ya muda mfupi, bali ni matunda ya awali ya mabadiliko ya kimfumo na ya kimuundo—mapinduzi ya kimya kimya yanayobadilisha kanuni za kile ambacho uchumi wa Afrika uliojaa rasilimali unaweza kufanikisha.
Msingi wa mabadiliko haya umejengwa juu ya mkutano wa sera za kimkakati, kukubaliwa na wadau kutoka nje, na fikra mpya kabisa kuhusu uwezo wa ndani ya nchi.
Utendaji mzuri wa sekta ya shaba, bidhaa kuu ya jadi ya kuuza nje ya Zambia, katika mwaka 2025 uliipa nchi ngao muhimu kwa kuongeza akiba ya fedha za kigeni. Hata hivyo, kuhusisha uimara mpya wa kwacha na faida ya bidhaa pekee ni kukosa kuona simulizi pana zaidi.
Mabadiliko ya kweli ulitokea Disemba 2025, pale Benki Kuu ya Zambia ilipotoa agizo kwamba miamala yote ya ndani ifanyike kwa kutumia kwacha. Huu ulikuwa uamuzi wa busara na uwazi mkubwa wa sera. Mara moja, uliweka kikomo kwa matumizi makubwa ya dola za kigeni ndani ya nchi ambayo kwa muda mrefu yalikuwa yakidhoofisha uhuru wa sera ya fedha, na kusababisha wimbi la kubadilisha dola kuwa kwacha.
Matokeo yalionekana wazi: sarafu iliamirikia hadi kiwango chake cha juu zaidi katika zaidi ya miaka miwili. Hatua hii ilithibitisha kanuni muhimu—kwamba sera iliyo wazi, thabiti na inayolenga maslahi ya taifa inaweza kuwa nanga madhubuti zaidi ya sarafu ya nchi, kuliko kutegemea matokeo ya masoko ya kimataifa yasiyotabirika.
Azma hii ya ndani iliimarishwa zaidi na kurejea kwa imani ya kimataifa. Ushirikiano endelevu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kupitia mpango wa mikopo uliweka mfumo wa nidhamu ya matumizi ya serikali.
Zaidi ya hayo, mwezi Novemba 2025, kuboreshwa kwa viwango vya mikopo ya taifa kutoka kwa mashirika kama Fitch na S&P hakukuwa marekebisho ya kiufundi tu; yalikuwa uthibitisho wa kimataifa kwamba safari ngumu ya Zambia ya kurekebisha madeni na mageuzi ya kifedha ilikuwa ikizaa matunda ya kuaminika.
Imani ya sarafu ya kwacha kutoka nje inapunguza mtazamo wa hatari na kuifanya nchi ivutie zaidi mitaji ya muda mrefu na yenye uvumilivu, badala ya mtaji wa kubahatisha unaosababisha kuyumba kwa uchumi.
Hata hivyo, hatua za kuvutia zaidi za mabadiliko haya zimefanikishwa katika mashamba na viwanda vya Zambia yenyewe. Kwa miaka mingi, sekta ya kilimo ilikuwa ishara ya udhaifu—kilimo cha kujikimu na utegemezi wa uagizaji wa msimu.
Simulizi hili sasa limegeuzwa kabisa. Uamuzi wa Baraza la Mawaziri kuruhusu usafirishaji wa zaidi ya tani 500,000 za mahindi ya ziada ni mabadiliko makubwa ya kimfumo. Kilimo si mzigo tena kwa akiba ya fedha za kigeni, bali ni chanzo kinachokua cha mapato ya kigeni.
Kwa kutumia kimkakati mahitaji ya chakula katika kanda, Zambia inageuza uwezo wake wa kiikolojia wa kilimo kuwa nguvu halisi ya kiuchumi, na kupanua misingi ya mapato yake ya fedha za kigeni.
Hili linatupeleka kwenye mojawapo ya ushindi wa kiuchumi usioripotiwa sana katika historia ya kisasa ya Zambia: mapinduzi ya kimya kimya katika uzalishaji wa mbolea. Kihistoria, nchi ilikuwa ikipoteza takriban dola za Kimarekani milioni 600 kila mwaka kuagiza mbolea—upotevu wa kimuundo uliokuwa ukiweka shinikizo la kudumu kwa kwacha.
Leo, kupitia uwekezaji na msaada wa sera kwa uzalishaji wa ndani, Zambia imegeuka kuwa muuzaji halisi wa mbolea kwa kanda. Huu ni ushindi wa njia tatu wenye umuhimu mkubwa.
Kwanza, unaokoa moja kwa moja mamia ya mamilioni ya dola zilizokuwa zikitoka nje kila mwaka. Pili, umechochea uundaji wa ajira na maendeleo ya viwanda ndani ya nchi. Tatu, na muhimu zaidi, umeimarisha kwa kiasi kikubwa usalama wa chakula kitaifa na kikanda kwa kulinda mlolongo wa thamani ya kilimo dhidi ya mishtuko ya bei za kimataifa na misukosuko ya usambazaji, kama ilivyoshuhudiwa wakati wa mzozo wa Ukraine.
Hatua hii ya kutoka kwenye udhaifu kwenda kujitegemea katika wakati muhimu ni tafsiri halisi ya mabadiliko ya kimuundo ya uchumi.
Katika kipindi chote hiki, Benki Kuu ya Zambia imetoa kipengele muhimu cha uongozi unaoaminika: uthabiti. Kwa kudumisha sera thabiti ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kuwasiliana hatua zake kwa uwazi, benki kuu imehakikisha kwamba misingi imara ya uchumi inatafsiriwa kuwa utulivu wa kudumu, si mabadiliko ya muda mfupi. Uthabiti huu hujenga imani ya umma, ambayo ndiyo msingi wa sarafu yoyote imara.
Kwa hiyo, tunachoshuhudia si kiwango tu kizuri cha ubadilishaji wa fedha. Tunashuhudia sarafu inayostahili nguvu yake.
Uimara wa kwacha katika msimu wa sikukuu ni ishara yenye nguvu ya mabadiliko mapana ya kitaifa. Unajengwa juu ya nguzo tatu: sera makini za uchumi mpana, upanuzi mkali wa mauzo ya nje, na uingizwaji wa kimkakati wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kuelekea kujitegemea.
Inaonyesha kwamba njia ya uhuru wa kiuchumi haijengwi kwa kujitenga kwa ajili ya kijikinga, bali kwa ujumuishaji wa busara—kuzalisha kile unachoweza, uuzaji wa nje wa kimkakati, na kusimamia fedha zako kwa nidhamu.
Changamoto iliyopo sasa ni kuimarisha kasi hii iwe ya kudumu. Safari iliyo mbele inahitaji kuendeleza mafanikio haya kwa kuongeza thamani katika sekta ya shaba (badala ya kuuza malighafi tu), kuhamasisha mauzo mengine yasiyo ya jadi, na kuhakikisha kwamba utulivu wa kwacha unatafsiriwa kuwa gharama ndogo za mtaji kwa biashara ndogo na za kati.
Upepo umebadilika kweli. Yaliyotokea Zambia ni funzo muhimu kwa bara zima: kwamba kwa sera zenye maono, nidhamu ya kifedha, na msisitizo usioyumba wa kufungua uwezo wa uzalishaji wa ndani, mzunguko wa udhaifu unaweza kuvunjwa.
Kwacha iliyoimarika si takwimu tu ya fedha; ni tamko la dhamira ya kiuchumi, na inaendelea kuimarika.
Mwandishi, Kennedy Chileshe, ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jubilee Leaders Network, shirika la utetezi wa sera na uongozi lenye makao yake Lusaka, Zambia.
Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayaakisi maoni, misimamo au sera za uhariri za TRT Afrika.













