Katika hatua iliyolaaniwa vikali kimataifa wiki iliyopita, Israel ikawa nchi ya kwanza kuitambua rasmi Somaliland kama taifa huru lenye mamlaka kamili.
Ingawa ilijitenga na Somalia mwaka 1991, nchi inayojiita Somaliland katika Pembe ya Afrika haitambuliwi na Umoja wa Mataifa wala Umoja wa Afrika. Serikali ya Somalia inaichukulia Somaliland kama sehemu isiyotenganishwa ya eneo lake.
Mbali na kuongeza hofu kwamba hatua ya Israel ni sehemu ya mkakati wa kuwalazimisha Wapalestina wahamishwe kutoka Gaza kwenda Somaliland, imeibua tena mjadala mwingine: je, tamaa za Kizayuni zinafika hadi nje ya Palestina?
Kwa wengi nchini Somalia na kwingineko, kitendo hiki cha kutambua si ishara ya kawaida ya kidiplomasia.
Maandamano yalizuka Mogadishu na miji mingine ya Somalia baada ya tangazo la Israel, huku waandamanaji wakipiga kelele za kudai umoja wa kitaifa na kupeperusha bendera za Palestina kama ishara ya mshikamano.
Hii ni kwa sababu wanaona hatua ya Israel kama mwendelezo wa mtindo wa Kizayuni wa kunyakua ardhi na kuunda upya idadi ya watu, ambao kihistoria ililenga hata maeneo ya mbali wakati upatikanaji kamili wa ardhi ya Palestina ulipoonekana kuwa na mashaka.
Huku nyaraka zinazosambaa mtandaoni zikionyesha pendekezo la miaka ya 1940 linalohusishwa na kile kinachoitwa Baraza la Harrar, wachambuzi wanajiuliza kama kutambuliwa ghafla kwa Somaliland na Israel ni sehemu ya mpango wa Kizayuni wa takribani miaka 80 wa kudhibiti ardhi ya kimkakati barani Afrika—huenda sasa kama eneo la kuwapeleka Wapalestina waliofurushwa.
Hati ya mwaka 1942 iliyoandikwa na mwanaharakati Myahudi Hermann Fuernberg ilizungumzia kuwahamisha Wayahudi wa Ulaya katika eneo la Harrar nchini Ethiopia, huku ikitumia bandari za Somaliland iliyokuwa chini ya ukoloni wa Uingereza iliyo jirani kwa ajili ya upatikanaji wa bahari.
“Pendekezo langu ni kuunganisha kile kinachoitwa eneo la Harrar la Ethiopia na sehemu ya Somaliland iliyokuwa chini ya ukoloni wa Uingereza na kuunda dola kwa ajili ya Wayahudi wa Ulaya,” aliandika Fuernberg, akiongeza kuwa wakazi wa eneo hilo la Afrika “huenda wasisababishe matatizo makubwa.”
“Kila Myahudi, awe anajiona hivyo au ameainishwa hivyo bila ridhaa yake, anapaswa kuwa na haki ya kuingia katika dola hii,” alisema.
Ingawa wazo hilo lilibaki pembeni, linaonyesha utayari wa mapema wa Kizayuni kutamani ardhi za mbali kwa namna ya ukoloni wa walowezi, kubadili idadi ya watu kupitia uhamiaji mkubwa wa Wayahudi ili kuanzisha utawala juu ya wakazi wa asili.
Vivyo hivyo, taarifa ya Februari 10, 1939 katika gazeti la The Canadian Jewish Chronicle ilitoa wito wa kuanzishwa kwa makazi ya Wayahudi nchini Ethiopia kwa sababu “tangu zama za Mafarao imekuwa na uhusiano na historia ya Kiyahudi.” Gazeti hilo limekuwepo tangu mwaka 1914.
“Ukanda mwembamba wa ardhi kati ya Mto Jordan na Bahari ya Mediterania—ambao sasa una Wayahudi nusu milioni na Waarabu milioni moja—hauwezi kabisa kutoshea Wayahudi wanaotishiwa na uhamisho leo,” ilisema, ikiongeza kuwa eneo la Afrika linapaswa “kufunguliwa kwa ukoloni wa Wayahudi.”
“Ethiopia, yenye udongo wake wenye rutuba ya nyanda za juu, na rasilimali zake ambazo bado hazijaendelezwa, inahitaji wakoloni… Ingempa Myahudi makazi ambayo hajawahi hata kuyaota katika ndoto zake,” iliongeza.
Aidha, taarifa za kila siku ya jukwaa la habari la Jewish Telegraphic Agency ya Julai 22, 1943 ilitangaza kuundwa kwa Baraza la Jimbo Huru la Kiyahudi katika eneo la Harrar.
Lengo lililotajwa la shirika hilo lilikuwa kusaidia Wayahudi wa Ulaya kuhamia katika eneo la Harrar nchini Ethiopia na katika Somaliland iliyoko chini ya ukuloni wa Uingereza amabayo ilikuwa ni jirani “chini ya masharti ya uhuru wa kisiasa.”
Tukiangalia mwaka 2025, hila na tamaa za Kizayuni za kunyakua ardhi bado zinaendelea kusikika.
Tangazo la Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, lililotolewa wakati wa mazungumzo ya simu na rais anayejiita wa Somaliland, Abdirahman Mohamed Abdullahi, lilitambulishwaa kama kupanua ushirikiano katika kilimo, afya na teknolojia.
Hata hivyo, Somalia na nchi nyingi zinahisi kuna nia zilizojificha, kwani hatua hiyo ya kidiplomasia inaendeleza malengo ya kijeshi ya Israel katika Bahari ya Shamu.
Wachambuzi wanasema ushirikiano wa Israel na Somaliland utaiwezesha Israel kupata ufikiaji wa kimkakati wa Mlango wa Bab el Mandeb, njia ya maji yenye upana wa kilomita 32 kati ya Rasi ya Arabia na Afrika, inayounganisha Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, njia muhimu ya safari za baharini.
Cha kutia wasiwasi zaidi, ripoti za mapema mwaka 2025 zilionyesha kuwa Israel na Marekani ziliwasiliana na Somaliland—pamoja na nchi nyingine kama Sudan, Somalia, Ethiopia, Libya na Indonesia—kuhusu kuwahamisha takribani Wapalestina milioni mbili waliokimbizwa na vita vya Gaza.
Wizara ya mambo ya nje ya Palestina iliunga mkono Somalia huku ikilaani Israel kwa kuzingatia Somaliland kama makazi ya Wapalestina walifurusha kutoka Gaza. Maafisa wa Somalia pia waliishutumu Israel kwa kutumia utambuzi huo kuwezesha utokomezaji wa kikabila huko Gaza, kuacha ardhi wazi kwa makazi ya Kiyahudi na kuwahamisha Wapalestina ili kubadili idadi ya watu barani Afrika.
Umoja wa Nchi za Kiarabu, Umoja wa Afrika, Misri, Uturuki, Saudi Arabia na mataifa mengine mengi pia yamekataa kutambuliwa kwa Somaliland na Israel, yakionya wazi kwamba kunaweza kuwezesha uhamisho wa kulazimishwa wa Wapalestina, sera ambayo wakosoaji wanaielezea kama utokomezaji wa kikabila.














