Utajiri wa Afrika: Uzalishaji wa mafuta Libya warejea
Meli ya mafuta ikiondoka kwenye kituo cha mafuta cha Zueitina, Libya baada ya mauzo ya mafuta kuanza tena Zueitina / Reuters
Utajiri wa Afrika: Uzalishaji wa mafuta Libya warejea
Mwaka 2025, Libya ilizalisha wastani wa juu zaidi wa mafuta ghafi katika zaidi ya muongo mmoja, na kufikia takriban mapipa milioni 1.37 kwa siku.
8 Januari 2026

Baada ya kumteka nyara na kumkamata rais wa Venezuela Nicolas Maduro, Marekani imesema kwamba itadhibiti uzalishaji wa mafuta nchini humo na "kufufua" uwezo wa nchi hiyo wa kuzalisha mafuta.Kauli hii imeibua mjadala kuhusu umuhimu wa mafuta katika siasa za kimataifa. 

Rasilimali hii ya mafuta, Afrika pia imejaaliwa kuwa nayo kwa wingi.Kwa jumla Afrika inaripotiwa kuwa na zaidi ya mapipa bilioni 125 ya mafuta yaliyothibitishwa.

Libya ikiwa inaongoza katika orodha hiyo ambapo inakadiriwa kuwa na takriban mapipa bilioni 48.36, hiki ni kiwango kikubwa zaidi barani Afrika.

Mwaka 2025, Libya ilizalisha wastani wa juu zaidi wa mafuta ghafi katika zaidi ya muongo mmoja, na kufikia takriban mapipa milioni 1.37 kwa siku.

Hili ni ongezeko kubwa kubwa kwa nchi hiyo ya Afrika Kaskazini. Kabla ya machafuko ya 2011 ambayo yalisababisha kupinduliwa na kuanguka kwa utawala wa Muamar Gaddafi na hatimae kuibuka vita vya wenyewe kwa wenyewe- nchi hiyo ilikuwa ikizalisha wastani wa mapipa milioni 1.6 hadi milioni 1.7 kwa siku.

Lakini baadae uzalishaji ukapungua.

Pato la taifa la mafuta nalo likapungua hadi kufikia mapipa 20,000 kwa siku. 

Vizuizi vya makundi yenye silaha, ushindani wa kisiasa, na hujuma dhidi ya miundombinu vyote vilichangia.

Serikali inasema ufufuaji wa uzalishaji karibu miaka 15 baadaye umechangiwa na uimarishaji mpana wa maeneo muhimu ya mafuta, vituo vya usafirishaji nje, na vifaa vya uendeshaji chini ya usimamizi wa Shirika la Mafuta la Kitaifa.

Mwaka 2025, kulikuwa na hali ya matumaini, ambapo maeneo ya mafuta na vituo vya usafirishaji vilianza kufanya kazi bila usumbufu mkubwa, ikisaidiwa na ukarabati wa miundombinu, kuimarika kwa hali ya usalama, na maboresho ya kiufundi.Mafuta ni uti wa mgongo wa uchumi wa Libya, na huchangia zaidi ya asilimia 90 ya pato la taifa.

Makampuni makubwa ya mafuta kutoka nchi za magharibi nayo yanaripotiwa kuanza kurudisha uwekezaji wake nchini Libya.

Shell na BP kwa mfano zimetia saini makubaliano na Shirika la Mafuta la Libya kutathmini fursa za utafiti, wakati ExxonMobil imeingiza mipango ya utafiti wa kiufundi.

Chevron pia inaripotiwa kuthibitisha mipango ya kurudi Libya baada ya kuondoka nchini humo mwaka 2010.

Libya ipo katika sehemu muhimu kijiografia. Iko kaskazini mwa Afrika, na pia ni lango la bara Ulaya.

Ukaribu wake wa kijiografia na Ulaya hupunguza zaidi gharama za usafirishaji ikilinganishwa na wasambazaji wengi wa Mashariki ya Kati au Afrika Magharibi.

Iwapo nchi hiyo itapata utulivu wa kudumu, basi matarajio yake ni kuzalisha zaidi ya mapipa milioni 2 kwa siku katika miaka ijayo.