Sirikit, mama yake Mfalme wa Thailand Vajiralongkorn, alifariki jijini Bangkok. Alikuwa na umri wa miaka 93.
Alifariki akiwa hospitali saa tatu na dakika ishirini na moja siku ya Ijumaa, kulingana na taasisi inayoshughulikia masuala ya Kifalme.
Iliongeza kuwa kundi la madaktari ambalo limekuwa likifuatilia afya yake tangu Septemba 7, 2019, lilimpata akiugua maradhi kadhaa na kutaka awe chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari.
Madaktari wanasema Sirikit alipatikana na matatizo kwenye mfumo wake wa damu Oktoba 17, na licha ya kutibiwa, hali yake ikaendelea kuwa mbaya.
Sirikit alikuwa mke wa Mfalme wa Thailand aliyekuwa mamlakani kwa muda mrefu zaidi, Mfalme Bhumibol Adulyadej, aliyefariki dunia 2016.
Mfalme Vajiralongkorn ametangaza mwaka mmoja wa maombolezo kwa familia ya Kifalme na maafisa wanaofanya kazi katika Kasri, kuanzia siku ya kifo cha Sirikit.
Tarehe ya kuzaliwa ya Sirikit inaadhimishwa kama Sikukuu ya kina Mama nchini Thailand na pia ni siku ya mapumziko kitaifa.











