Wizara ya Mambo ya Ulinzi ya Uturuki imesema siku ya Jumanne kuwa ndege ya Uturuki iliyopata ajali karibu na mpaka wa Georgia na Azerbaijan ilikuwa na watu 20 raia wa Uturuki, wakati ikitokea Azerbaijan kuelekea Uturuki.
Katika taarifa yake ya awali, wizara hiyo ilisema kuwa ndege hiyo ilitoka Azerbaijan kuja nchini kwetu kabla haijapata ajali kwenye mpaka wa Georgia na Azerbaijan,” ikiongeza kuwa shughuli za uokozi zinaendelea chini ya uratibu wa mamlaka za Azerbaijan na Georgia.
Hakuna taarifa zozote zilizotolewa kuhusu vifo au majeruhi wa tukio hilo.
Rais Recep Tayyip Erdogan alisema kuwa alihuzunishwa sana na tukio hilo, akiongeza kuwa shughuli za kufikia eneo hilo zinaendelea.
“Kazi yetu inaendelea chini ya uratibu wa mamlaka husika. Mungu awarehemu mashahidi wetu,” alisema Erdogan kupitia mtandao wa X.
Kulingana na wizara hiyo, uchunguzi wa kujua chanzo cha tukio hilo umeanza.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya alisikitishwa na tukio hilo kupitia mtandao wa wa kijamii wa NSosyal.
Yerlikaya alisema kuwa alijadiliana kuhusu tukio hilo kwa njia ya simu na mwenzake wa Georgia Gela Geladze, ambaye alisema alikuwa anaelekea eneo la tukio.
Kupitia mtandao wa NSosyal, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Uturuki Burhanettin Duran alisema kuwa shughuli ya uokozi na utafutaji ilikuwa inaendelea kwa kasi.
“Ili kuhakikisha kuwa tuna taarifa sahihi, tunatoa wito kwa umma kuamini tu taarifa zinazotolewa na mamlaka rasmi na kupuuzia taarifa potofu,” aliongeza.
Jitihada za uokozi za Georgia
Kulingana na vyanzo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan alikuwa na mazungumzo ya simu na mwenzake wa Georgia, Maka Botchorishvili, kuzungumzia jitihada za uokozi.
Botchorishvili pia alituma salamu zake za rambirambi kufuatia ajali hiyo.
Kwa upande wake, mamlaka ya usalama wa anga ya Georgia Sakaeronavigatsia ilisema kuwa ndege hiyo ilipata ajali karibu na mpaka na Azerbaijan.
Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Facebook, mamlaka hiyo ilisema kuwa ndege hiyo ilipotea kutoka kwenye rada, dakika chache baada ya kuvuka eneo la Georgia bila kutuma ujumbe wowote.
Rambirambi kutoka Azerbaijan
Kufuatia tukio, Rais wa Azarbaijan Ilham Aliyev alikuwa na mazungumzo ya simu na mwenzake wa Uturuki na kutuma salamu zake za rambirambi kufuatia tukio hilo.
"Wakati wa mazungumzo hayo, ilitaarifiwa kuwa mamlaka za Azerbaijan na Uturuki walikuwa pamoja kushughulikia tukio hilo," ilisema taarifa hiyo.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Uturuki Cevdet Yilmaz alikuwa na mazungumzo na Waziri na Waziri Mkuu wa Azerbaijan Ali Asadov, kuhusu tukio hilo.
Kupitia ukurasa wa NSosyal, Yilmaz alisema kuwa Asadov alituma salamu za rambirambi kutoka Azerbaijan na kusisitiza kuwa nchi hiyo inafuatilia hali hiyo.
Yilmaz alimshukuru kiongozi wa Azerbaijan kwa sala na matashi yake.



























