Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameapishwa siku ya Jumatatu kwa muhula wake wa kwanza wa kuchaguliwa baada ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi uliozua maandamano makubwa kote chini.
Alikula kiapo katika sherehe rasmi za kijeshi kwenye mji mkuu wa Dodoma.
Samia, ambaye aliingia madarakani mwaka 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake, alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa wiki iliyopita kwa asilimia 97.66 ya kura.
Samia mwenye umri wa miaka 65, alikabiliana na wagombea kutoka vyama vidogo baada ya wapinzani wake wakuu kutoka vyama viwili vikuu vya upinzani kuondolewa kwenye kinyang'anyiro hicho.
Maandamano yalizuka wakati wa wananchi wakipiga kura Jumatano iliyopita, huku baadhi ya waandamanaji wakichoma moto majengo ya serikali na polisi wakifyatua mabomu ya machozi na milio ya risasi kusikika, kulingana na walioshuhudia.
Chama kikuu cha upinzani kimesema mamia ya watu wameuawa katika maandamano hayo, huku ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ikisema ripoti za kuaminika zinaonyesha kuwa watu wasiopungua 10 waliuawa katika miji mitatu.
Serikali ilijitetea ikieleza kupinga idadi ya vifo iliyotolewa na vyama vya upinzani.








