Huku teknolojia ya blockchain ikiendelea kutawala majukwaa ya kidijitali duniani, Bara la Afrika lingali bado kukumbatia teknolojia hio kwa ukamilifu.
Hatahivyo mambo yameonekana kubadilika ndani ya miaka miwili iliyopita huku teknolojia ya blockchain ikipiga jeki harakati zake katika bara hilo.
“Afrika inajenga kwa kasi sifa ya uwezekano wa kuwa kitovu muhimu cha sarafu ya kidijitali ‘crypto’ ulimwenguni.” Anaiambia TRT, Gideon Greaves, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Crypto Valley Venture(CV VC) katika bara la Afrika.
“Sarafu ya kidijitali kwa sasa inaanza kuvuma!”
Teknolojia ya blockchain inatoa fursa ya uwezekano mpya wa kusuluhisha mambo kwa njia salama na iliyo na uwazi na zaidi pia njia isiyohitaji mhusika wa kati. Kutokana na hali hiyo basi sarafu a kidijitali imeteka macho ya watu wengi wakionesha sasa kutaka kufahamu teknolojia hiyo zaidi.
Sasa hivi bara la Afrika ni la tatu kiukubwa katika ukuaji wa sarafu hii ya mtandaoni na teknolojia ya blockchain kwa ujumla. Upitishaji wa sarafu ya crpto Afrika uliongezeka kwa zaidi ya asilimia 1,200 kati ya Julai 2020 na Juni 2021.
Viwango vya upitishaji viko juu zaidi katika baadhi ya nchi kama vile Kenya, Afrika Kusini, Tanzania na Nigeria, ambapo uhaba wa miundombinu madhubuti ya kutoa huduma za kifedha ni tatizo na hivyo basi crypto inaonekana kurahisisha mambo. Aidha mwezi Aprili Jamhuri ya Afrika ya Kati ilipitisha Bitcoin(BTC) na kuitambua kama zabuni halali, ikiwa ndiyo nchi ya pili kufanya hivyo baada ya El Salvador.
Kwenye ripoti iliyochapishwa na CV VC wiki iliyopita, kampuni za teknolojia ya blockchain katika bara la Afrika zilikusanya dola za kimarekani milioni $91 katika robo ya kwanza yam waka wa kifedha 2022, ambayo ni ongezeko la asilimia 1,668 la mzunguko wa pesa ikilinganishwa na robo ya kwanza yam waka wa kifedha 2021 ambapo ukuaji ulikuwa ni asilimia 149.
Kiasi cha dola za kimarekani milioni 127$ zilikusanywa mwaka wa 2021, hii ikiwa ni asilimia 0.5% ya ufadhili wa blockchain kote ulimwenguni. Asilimia 96% ya dola hizo za ubia yaani ‘venture dollars’ ziliendea Kenya, Afrika Kusini na Ushelisheli. Kwenye zilizokusanywa, biashara za fintech zilihesabiwa kuwa dola milioni 67(sawa na asilimia 53) ya ufadhili mzima wa blockchain huku kubadilishana kwa sarafu kukihesabiwa kuwa dola milioni 34(asilimia 26).
Mpaka kufikia sasa mfumo wa kifedha umeanza vizuri katika robo ya kwanza ya 2022, kampuni ya kubadilisha sarafu MARA ikikusanya dola milioni 23 mwezi uliopita; Jambo ambayo ni kampuni ya program ikiingiza dola milioni 30 huku Afriex kutoka Nigeria ikipata dola milioni 10.
Kwengineko VALR kutoka Afrika Kusini ilikaribia kubuni dili kubwa ya kihistoria ya blockchain kwa kuingiza dola milioni 50 kwenye msururu B mwezi Machi, ambao ni ufadhili mkubwa zaidi katika Bara la Afrika mpaka kufikia sasa.
Na licha ya kuwa bado hakuna ‘unicorn’ za sarafu ya crpto na blockchain ambazo zimeibuka Afrika, inatarajiwa kuwa zitaibuka katika kipindi cha miaka miwili au mitatu ijayo. Hatahivyo zipo ‘unicorn’ za teknolojia ambazo zimejumuisha blockchain kwenye biashara zao, zikiwemo kampuni ya Interswitch ya Nigeria pamoja na kampuni ya fintech iitwayo Wave ya Senegal.
“Makampuni mengi kutoka Afrika yanazidi kukumbatia teknolojia kwa kujiunga na klabu za ‘unicorn’ kimataifa na tunatarajia mengi zaidi.” Anasema Greaves ambaye anaamini kuwa Afrika itakuwa kipaumbele katika uwekezaji kwenye blockchain ndani ya muongo mmoja.
Uvumbuzi ni muhimu
Kuongezeka kwa teknolojia ya mawasiliano na simu barani Afrika kumechochea zaidi uelewa wa watu kuhusu sarafu ya mtandao na teknolojia ya blockchain na hilo litawapa watu tofauti mbadala wa walichokizoea. Takriban watu milioni 370 kutoka Afrika wanaaminika kutokuwa na akaunti za Benki na hivyo basi blockchain ni mbadala mzuri kwa idadi hiyo kubwa, ikiwemo uuzaji na ununuzi wa Bitcoin kwenye soko la Bitcoin kama vile Paxful na ‘localbitcoins’
Renata Rodrigues ambaye ni kiongozi wa huduma ya Paxful anatolea mfano Huduma ya M-Pesa kutoka Kenya ambayo imefanikiwa kupitiliza kote Afrika kwa kuwahusisha mamilioni ya watu. Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Kenya, miamala ya pesa kwa simu nchini humo iliongezeka kwa asilimia 32% mwaka wa 2021.
“Kupitia utoaji wa elimu ya kutosha kuhusu Bitcoin, tutaanza kuona mabadiliko kutoka kwa huduma za kijadi za fedha.” Anasema Rodrigues.
Aidha kuzuka kwa sarafu ya kidijitali na ubadilishanaji kamepelekea kuongezeka kwa teknolojia kama vile ya kadi ya njano yaani ‘Yellow card’ ambayo inatumika katika mataifa mengi na mpango wa kupanua ungalipo.
Kwa kuzingatia pia umuhimu wa Kilimo katika bara la Afrika, sio jambo la kushangaza kuwaona wakulima pia wakiikumbatia teknolojia ya blockchain. Mfano mmoja ni BeefLedger ya Afrika Kusini ambayo inatumia teknolojia ya blockchain kung’amua ubora wa bidhaa za nyama na utapeli wa biashara ya nyama ambao ni tatizo sugu nchini humo.
Aidha wadau katika uchimbaji madini nao hawajaachwa nyuma. Kampuni ya Uchimbaji madini De Beers ilizindua Tracr, ambayo ni sehemu ya blockchain inayosaidia kung’amua chanzo na ubora wa madini ya almasi.
Greaves anaamini kuwa mataifa ya Afrika yako kwenye nafasi nzuri kutumia vizuri teknolojia ya blockchain kwa manufaa yao.
“Waafrika wengi hawawezi kutegemea mfumo mmoja wa kifedha unaodhibitiwa kutoka sehemu moja. Mifumo ya aina hiyo mara nyingi hukumbwa na madhaifu. Kutokana na ukweli hio basi uvumbuzi umeleta mfumo mbadala.”
Kutoka Uswisi mpaka Afrika
Kampuni moja ya uwekezaji kutoka Uswisi, kwa kushirikiana na CV VC ina mpango wa kuzindua mfuko wa ufadhili kwa ajili ya kuwezesha makampuni 100 ya Afrika yatakayoshirikisha teknolojia ya blockchain kwenye shughuli zao. Takriban dola milionin 50 zimetengwa kwa ajili ya ufadhili huo kwa miaka minne ijayo.
Mfuko huo wa ufadhili tayari umewekeza kwenye makampuni kadhaa yakiwemo. Kampuni ya kidijitali ya HouseAfrica kutoka Nigeria and kampuni Mazzuma kutoka Ghana.
CV VC inaendelea kuwasiliana na washikadau tofauti wakiwemo wa Serikali na taasisi za elimu kuona ni jinsi gani teknolojia ya blockchain inaweza kuongeza tija kwenye harakati za kukuza uchumi na kubadilisha hali za maisha ya watu.
Ubalozi wa Uswisi nchini Afrika kusini umekuwa mshirika muhimu katika upatikanaji wa ushirikiano baina ya sekta kadhaa lengo kuu likiwa ni kubuni nafasi za biashara zitakazokumbatia teknolojia ya blockchain na kurahisisha namna ya kufanya kazi.
“Kwenye kufanya hilo ufadhili huo wa Uswisi utapata nafasi pia ya kufahamu kipi ambacho Afrika inaweza kutoa na kusaidia wengine.” Anaeleza Greaves.
“Masoko yanazidi kuongezeka kwa kasi kubwa hasa ndani ya Afrika. Ukosefu wa miundo mbinu madhubuti unatoa nafasi kwa uvumbuzi kuingia na kuja na mbinu mpya za kiteknolojia.” anaongeza Greaves.
Changamoto zilizoko na Suala la Sheria za Udhibiti
Licha ya kuwa nafasi ni nyingi kukumbatia uvumbuzi hasa wa teknolojia kama blockchain, ukweli ni kuwa zipo changamoto katika sekta mbalimbali.
Moja ya changamoto kubwa ni ubora wa mtandao na mawimbi ya intaneti katika baadhi ya mataifa. Ukubwa na ubora wa mtandao mpaka kwenye maeneo yaliyo kwenye mashinani ni asilimia 43 huku Benki ya Dunia ikikadiria kuwa huenda hilo likahitaji zaidi ya dola bilioni 100 kufikisha mtandao katika kila kona na huenda ikachukua zaidi ya mwongo mmoja kufanikisha hilo.
Hali kadhalika kuna sheria kandamizi za udhibiti zinazowazuia wanaotaka kujihusisha na sarafu ya kidijitali na teknolojia yake. Kati ya jumla ya nchi 54 za Afrika, 31 zimeweka marufuku ya sarafu za kidijitali huku nchi 17 zikiwa zimeweka sheria kandamizi za udhibiti ambazo hazifanikishi sarafu ya dijitali.
Afrika Kusini, ambalo ni taifa lililo na sekta endelevu kabisa za kifedha imefanikiwa kuweka sheria wazi juu ya sarafu ya crpto na kuweka sarafu mbili kuu za kidijitali lakini kwa uangalizi mkubwa.
Mauritius ilikuwa moja kati ya mataifa ya kwanza kukumbatia matumizi ya sarafu za kidijitali huku taifa la Ushelisheli tayari likiwa limeanza kuonesha nia ya kutunga sheria-rafiki za sarafu hiyo.
Kenya kwa upande wake imejitahidi kufanya vizuri na ipo katika nafasi ya tano katika kukumbatia sarafu ya kidijitali, na licha ya kuwa Kenya haijaweka kanuni kandamizi za kuhusu sarafu hii, Benki Kuu ya Kenya ipo makini sana kutupia jicho teknolojia ya crypto.
Katika mataifa kama Nigeria hakuna sheria inayozuia sarafu za kidijitali japokuwa serikali ya nchi hiyo iliweka kikwazo cha kuwakatisha tamaa wanaoitumia ila hilo lilionekana kutofanikiwa. Nigeria imekuwa taifa la kwanza Afrika kuzindua sarafu yake ya kidijitali eNaira mwezi Oktoba mwaka jana.
Licha ya kero la sheria za udhibiti, makampuni mengi yamezidi kushirikisha teknolojia ya blockchain katika kazi zao na tayari CV VC ilishatambua na kuchagua kampuni 41 zilizopata ufadhili kati ya Januari 2021 na Machi 2022.
“Afrika Kusini na Mauritius zimeonesha namna hatua endelevu za kukumbatia sarafu za kidijitali zinaweza kuwa na umuhimu mkubwa. Huu ndio mtazamo unaotufanya sisi kuwafuata.” Alisema Greaves.
“Kadri tu mwafaka kuhusu kanuni za udhibiti unapofikiwa, ndivyo tu basi uwezekano mkubwa unazidi kufurahisha.”