Uganda inapanga kukopa dola milioni 358 kutoka kwa wakopeshaji wa kikanda na binafsi kufadhili miradi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuunganisha gridi ya umeme na taifa jirani la Sudan Kusini.
Taarifa hii ni kulingana na afisa wa Wizara ya Fedha.
Mikopo hiyo itatolewa kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Afrika, tawi la Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika, na Benki ya Standard Chartered, itafungua ukurasa mpya, Waziri mdogo wa Fedha, Henry Musasizi, alisema wakati akiwasilisha mpango huo bungeni Jumanne.
Naibu Spika wa Bunge, Thomas Tayebwa alipeleka ombi hilo katika kamati ya Bunge, inayojumuisha wabunge wa vyama tawala na upinzani, ambayo italichunguza na kutoa ripoti kabla ya mjadala wa Bunge zima na kulipigia kura ombi hilo.
Miradi mingine itakayofadhiliwa na mkopo huo ni pamoja na barabara kaskazini magharibi mwa nchi inayounganisha Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na upanuzi wa maji safi.
Uganda, ambayo sasa inazalisha umeme wa ziada baada ya kuanzisha bwawa la kufua umeme wa maji kwa dola bilioni 1.7 mwaka jana, imekuwa ikipanga kuanza kusafirisha baadhi ya umeme wake wa ziada kwa Sudan Kusini yenye njaa ya nishati.