Biashara ya kahawa nchini Uganda inazidi kushamiri
Biashara ya kahawa nchini Uganda inazidi kushamiri
Nchi hiyo sasa imepita Ethiopia katika mauzo ya kahawa barani humo kulingana na ripoti za hivi punde za kahawa kutoka wizara ya kilimo nchini humo.
12 Septemba 2025

Na Eudes Ssekyondwa

Kampala, Uganda

Ibrahim Ssenyange ni mkulima wa kahawa nchini Uganda. Amekuwa akilima kahawa kwa miaka 10 iliyopita. Anasema baada ya muda mrefu sasa hivi ameanza kuona fursa kwa wakulima kama yeye kuongeza mapato

"Kama mkulima nimebaini kuwa kahawa yetu ina mahitaji makubwa,” Ssenyange anaiambia TRT Afrika.

“Sasa kuna uwezekano mkubwa wa kufaidika kwa sababu kahawa hiyo itauzwa kwa bei ya juu.”

Sio Ssenyange pekee mwenye matumaini ya kupata mapato zaidi. 

Jackie Arinda mchakataji kahawa pia ameanza kula matunda ya kazi hiyo.

 "Athari za kimataifa ni kuongezeka kwa ajira,” Jackie Arinda , mkurugenzi wa kampuni ya Jada Coffee anailezea TRT Afrika.

“Ongezeako la mapato ya kahawa imepelekea kuwepo kwa mikahawa zaidi na hivyo kuunda ajira. Ukienda China unasikia maelfu ya mikahawa inafunguliwa. Hii ni habari njema kwetu kwani watanunua zaidi,” anaongezea.

Ongezeko la mauzo

Mapato ya mauzo ya nje ya kahawa kila mwaka nchini Uganda yameongezeka kwa karibu asilimia 95 katika mwaka ulioishia Aprili 2025 na hadi kufikia dola bilioni 1.97.

Hii imechangiwa zaidi na ongezeko la bei ya kahawa kimataifa.

Takwimu za hivi karibuni kutoka Wizara ya Kilimo nchini humo, zinaonyesha kuwa nchi hiyo ilipata karibu dola milioni 245 mwezi Mei 2024 pekee baada ya kuuza nje magunia 793,445 ya kilo 60 ya kahawa.

"Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita Uganda imekuwa ikiongeza uzalishaji wa kahawa na mauzo ya nje ya nchi. Kwa kweli, tuna ongezeko la karibu asilimia 3 kila mwaka. Hivyo kila mwaka mauzo yetu ya nje yanazidi kukua.” Kenneth Barigye mtaalamu wa biashara aiambia TRT Afrika.

“Sababu kuu inayofanya mauzo ya kahawa ya Uganda kushinda Ethiopia hasa ni uwekezaji wa serikali katika sekta ya kahawa,” Barigye anasema.

Kiwango cha mauzo ya nje ya kahwa kutoka Uganda sasa kimepita kile cha Ethiopia ambayo awali ndio iliiyokuwa kinara wa uzalishaji wa kahawa na muuzaji mkubwa nje ya bara la Afrika.

Ongezeko kubwa la mapato limechangiwa zaidi na kupanda kwa bei ya kahawa kwenye soko la kimataifa, huku uzalishaji wa kimataifa ukiendelea kukandamizwa. 

Katika msimu uliopita, Brazil na Vietnam ambao ni wazalishaji wakubwa wa kahawa duniani walikuwa na mavuno machache baada ya mashamba kuharibiwa na ukame na baridi kali.

Mpango wa kuzalisha zaidi

Wachambuzi wa biashara wanasema inaweza kuchukua muda zaidi kwa wazalishaji wakuu duniani kurudi nyuma, jambo ambalo ni la manufaa kwa wazalishaji wa kahawa barani Afrika.

“Serikali imeweka mkazo mkubwa wa kuuza kahawa ya Uganda katika nchi nyingi zaidi, nchi ambazo hazikuwa wanunuzi wa kahawa ya Uganda, tumeona ongezeko la zaidi ya asilimia 2000 kwa sababu ya mpango wa serikali,” Barigye ameelezea.

Lengo la Uganda ni kuzalisha zaidi ya magunia milioni 20 ya kahawa ifikapo 2035.

Ili kushindana katika soko la kimataifa, serikali ya Uganda inawahimiza wakulima wake kudumisha ubora wakati wa maandalizi baada ya kuvuna. 

Nchi hii ya Afrika Mashariki inapanga kuboresha uzalishaji wake ili hata wakati wazalishaji wakubwa wa kahawa wakirudi sokoni, kahawa ya Uganda itakuwa tayari imekita mizizi katika soko, na wakulima kama Ssenyange wataendela kupata malipo mazuri zaidi.


CHANZO:TRT Swahili