Muungano wa wafanyakazi wa mafuta nchini Nigeria umekubali kusitisha mgomo baada ya mkutano na uongozi wa Dangote Petroleum pamoja na maafisa wa serikali, Wizara ya Kazi ya nchi hiyo imesema.
Mgomo huo ulianzishwa baada ya kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote - ambacho ni kikubwa zaidi barani Afrika na kina uwezo wa kusafisha mapipa 650,000 ya mafuta kwa siku - kuwasimamisha zaidi ya wafanyakazi 800 waliokuwa wamejiunga na muungano.
Hatua hiyo ya mgomo ilikuwa imeweka hatarini usambazaji wa mafuta na biashara katika eneo la Afrika Magharibi.
Wizara ya Kazi ilisema katika taarifa baada ya mkutano wa upatanishi kati ya muungano wa PENGASSAN na Dangote Petroleum kwamba wafanyakazi waliokuwa wamefukuzwa watapewa nafasi za kazi katika sehemu nyingine za kundi la Dangote bila kupoteza mishahara yao.
Waziri wa Kazi alisisitiza katika mkutano huo kwamba kujiunga na muungano ni haki ya wafanyakazi na inapaswa kuheshimiwa.
"PENGASSAN wamekubali kuanza mchakato wa kusitisha mgomo," taarifa hiyo iliongeza.
“Wafanyakazi katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote, ambacho kinamilikiwa binafsi, walifukuzwa kazi siku ya Alhamisi kwa sababu ya kujiunga na muungano, PENGASSAN,” ilisema siku ya Ijumaa.
Maafisa wa kiwanda cha Dangote walisema wakati huo kwamba kufukuzwa kazi kwa wafanyakazi hao kulikuwa sehemu ya mpango wa kupanga upya wafanyakazi na waliwatuhumu walioathirika kwa vitendo vya hujuma.