Waumini wa Kiislamu nchini Tanzania wameshiriki ibada ya Ijumaa katika misikiti mbalimbali kote nchini, huku ujumbe wa amani ukitawala katika ibada hizo.
Wakati huo huo, katika mawaidha yake, Sheikh wa Mkoa Dar es Salaam Walid Alhad Omar, ametilia mkazo suala la amani, akitolea mfano wa madhara ya vita vya Kagera vilivyopiganwa mwaka 1978 kati ya Tanzania na majeshi vamizi ya Idi Amin.
Akizungumza Oktoba 24, 2025, Sheikh Alhad amewataka waumini wa mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi siku ya Oktoba 29 kwa ajili ya shughuli ya upigaji kura, na kurejea majumbani mwao kwa amani.
“Nimesikiliza wagombea kutoka vyama 17, na ninazifahamu sera zao, ila niwatake tu mshiriki zoezi hilo kwa amani, tukikumbuka yale yaliyotokea wakati wa uvamizi wa Idi Amin mwaka 1978,” amesema Sheikh huyo.
Kwa mujibu wa Sheikh Alhad, madhara ya vita hivyo, maarufu kama ‘Vita vya Kagera’, vilikuwa na matatizo makubwa, vikisababisha vifo na majeruhi kwa raia wa Tanzania na Uganda, hivyo ni vyema kuimarisha amani iliyopo nchini Tanzania, hata baada ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.










