Mpango wa kufunguliwa upya kwa uwanja mkuu wa ndege wa Sudan mjini Khartoum baada ya kufungwa kwa miaka miwili na nusu umerudishwa nyuma.
Hii ni baada ya kikosi cha wapiganaji wa RSF kushambulia uwanja huo kutumia ndege zisizo na rubani asubuhi ya Jumanne.
Uwanja wa ndege ulio katikati mwa mji mkuu wa Sudan ulishambuliwa mwanzoni mwa vita kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya RSF, na kusababisha uharibifu mkubwa kwa majengo yake na kusimamishwa mara moja kwa safari za ndege.
Kufuatia kuchukua udhibiti tena wa mji wa Khartoum mapema mwaka huu, serikali inayoongozwa na jeshi ilifanya ukarabati na kuanzisha upya uwanja huo kuwa mojawapo ya vipaumbele vyake vya juu kuashiria kurejea kwa maisha ya kawaida katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wake.
Zaidi ya watu milioni 1 wamerejea katika mji mkuu, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji linasema, baada ya mamilioni kuondoka baada ya Vikosi vya RSF kuchukua udhibiti wa mji huo.
Udhaifu wa uwanja wa ndege
Ndege ya safari za ndani ya kwanza ya kibiashara ya kampuni ya Badr Airlines ilipangwa kufanyika Oktoba 22, lakini mashambulizi ya ndege zisizo na rubani mapema Jumanne na Jumatano yaliashiria kuendelea kwa udhaifu wa uwanja huo.
RSF imeshambulia miundombinu ya kijeshi na ya kiraia katika maeneo yote yanayodhibitiwa na jeshi kwa kutumia ndege zisizo na rubani wakati ikipigania kuimarisha udhibiti wa eneo la Darfur.
Chanzo cha shirika la ndege kilisema safari hiyo ilicheleweshwa kwa siku kadhaa kwa sasa, huku hali ikiendelea kufuatiliwa.
Mapema wiki hii, kampuni hiyo ilisema kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook kwamba ilikuwa imefanya majaribio ya ndege katika uwanja huo. Na kwamba ndege za safari za ndani pekee ndizo zimepangwa kwa wakati huu.
Mkuu wa jeshi na kiongozi wa Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alizuru uwanja wa ndege siku ya Jumanne baada ya mashambulizi hayo, hata hivyo taarifa ya jeshi ilisema mashambulizi hayo yaliweza kuzuiwa.
Vyanzo vya usalama vilisema uharibifu kutoka kwa mashambulizi ya siku zote mbili ulikuwa mdogo.