Polisi nchini Uingereza walisema kuwa aliyekuwa mwanamfalme, Andrew Mountbatten-Windsor, amekamatwa kwa tuhuma za utovu wa nidhamu akiwa mtumishi wa umma wakati alipohudumu kama balozi wa biashara.
Polisi hawakutaja jina lake hadharani. Hata hivyo, walipoulizwa kama Andrew amekamatwa, waliashiria taarifa yao iliyosema kuwa wamemkamata mwanamume mwenye umri wa miaka sitini na zaidi.
“Katika hatua ya uchunguzi huu, leo (tarehe 19 Februari) tumemkamata mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka sitini kutoka Norfolk kwa tuhuma za utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma,” ilisema taarifa ya Polisi wa Thames Valley.
“Baada ya tathmini ya kina, sasa tumefungua rasmi uchunguzi kuhusu madai haya ya utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma,” iliongeza taarifa hiyo.
“Ni muhimu kulinda uadilifu na uhuru wa uchunguzi wetu tunaposhirikiana na wadau wetu kuchunguza tuhuma hizi.”
Polisi pia walisema maafisa wao walikuwa wakifanya upekuzi katika anwani mbili moja mashariki mwa Uingereza na nyingine magharibi mwa London.
Taarifa mpya zilizotolewa wiki iliyopita zimebainisha kuwa Andrew alimtumia mhalifu wa makosa ya kingono aliyetiwa hatiani, Jeffrey Epstein, nyaraka ambazo huenda zilikuwa za siri, wakati alipokuwa akihudumu kama balozi wa biashara wa Uingereza.

















