| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Zaidi ya Wakenya 1,000 washiriki katika vita vya Urusi na Ukraine
Idara ya Kijasusi ya Kenya, imeliarifu bunge la nchi hiyo kuwa, zaidi ya Wakenya 1,000 wanapigana upande wa Urusi katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine, jambo linalozua wasiwasi mpya kuhusu kuajiriwa kwa raia kwenda mataifa ya kigeni na usalama w
Zaidi ya Wakenya 1,000 washiriki katika vita vya Urusi na Ukraine
Serikali mbalimbali barani Afrika na Asia zimewahi kuwaonya raia wao dhidi ya kujiunga na mzozo huo. / / AA
tokea masaa 16

Maafisa kutoka Idara ya Kitaifa ya Ujasusi walitoa taarifa hiyo wakati wa kikao cha bunge jijini Nairobi siku ya Jumatano, wakionya wabunge kuhusu kuongezeka kwa idadi ya raia wanaoaminika kusafiri nje ya nchi kujiunga na mzozo huo unaoendelea.
Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na maafisa wa ujasusi zinaonesha ongezeko kubwa, ikilinganishwa na mwezi Novemba mwaka jana.

Akizungumza bunge mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, alisema kuwa takriban Wakenya 200 walikuwa wanapigana kwa niaba ya Urusi katika mzozo huo.

Kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa, Kimani Ichung’wah, aliliambia bunge kwamba juhudi zaidi zinahitajika ili kuwalinda Wakenya dhidi ya mbinu za udanganyifu za kujiriwa nje ya nchi.

Alihimiza kuimarishwa kwa usalama mipakani na uchunguzi wa kina zaidi wa safari za wanaoondoka nchini ili kubaini ni nani anaondoka na kwa sababu gani.

Kwa mujibu wa maafisa wa usalama, mashirika ya kuajiri yasiyo na leseni ndiyo yanalaumiwa kwa kiasi kikubwa, huku baadhi yao yakifanya kazi nje ya mfumo rasmi wa usimamizi na kudaiwa kuwalaghai wanaotafuta ajira kwa ahadi za kazi za usalama au ujenzi nje ya nchi.

Mamlaka zilisema kuwa waajiriwa wengi husafiri kupitia nchi nyingine za Afrika kabla ya kufika Urusi, jambo linalofanya juhudi za ufuatiliaji kuwa ngumu zaidi.

Serikali mbalimbali barani Afrika na Asia zimewahi kuwaonya raia wao dhidi ya kujiunga na mzozo huo, zikionya kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kisheria, kidiplomasia na kiusalama.

Mamlaka za Kenya zimekuwa zikiwashauri mara kwa mara raia kuthibitisha fursa za ajira za nje ya nchi na kuepuka mipango ya kuajiriwa inayohusishwa na migogoro ya kijeshi.

Maafisa wanasema baadhi ya waajiriwa huenda wasitambue kuwa wanaingia katika majukumu ya mapigano hadi wanapoondoka nchini, jambo linalofanya iwe vigumu kuwafuatilia na kuwasaidia.

CHANZO:AA