Mlima wa volkano katika Mkoa wa Afar nchini Ethiopia, Erta Ale hivi majuzi ulilipuka na kutoa majivu, huku wataalamu wakisema ulikuwa mlipuko wa kwanza wa aina hiyo baada ya zaidi ya miaka 10,000.
Erta Ale ni mojawapo ya maajabu ya asili ya kuvutia zaidi ya bara.
Volkano hii ina ziwa la lava lisilobadilika ambalo limevutia wanasayansi na wavumbuzi. Mazingira magumu ya maajabu haya ya kijiolojia, ambayo mara nyingi hujulikana kama "Lango la Kuzimu," inaongeza hali yake ya upekee.
Barani Afrika kuna baadhi ya volkano za ajabu zaidi duniani likiripotiwa kuwa na zaidi ya volkano 100 ambazo zinaweza kulipuka wakati wowote.
Tuangazie volkano kadhaa.
Volkano za Tanzania
Mlima Kilimanjaro, uliopo nchini Tanzania pia unajulikana kama ‘Paa la Afrika’.
Una urefu wa mita 5,895, na unatambulika kwa kuwa kilele cha juu zaidi barani Afrika.
Wataalamu wanasema ulilipuka zaidi ya miaka 200,000 iliyopita, na sasa unajulikana kama volkano iliyotulia.
Hapo tu tanzania kuna Mlima Meru, umeripotiwa kuwa na milipuko minne, ambapo mara ya mwisho ulitokea mwaka wa 1910. Kilimanjaro imefunika sifa ya Mlima Meru lakini licha ya hayo, mlima huo unawapa wanaopanda mlima mazingira magunu lakini ya kuridhisha kwa wanaopenda shughuli hizi.
Mlima wa volkano Ol Doinyo Lengai pia unapatikana nchini Tanzania. Miongoni mwa watu wa jamii ya Wamasai, wanauita "Mlima wa Mungu," wakitoa heshima kwa ubunifu usio na kifani wa asili.
Ol Doinyo Lengai ni wa kipekee kutokana na kuwa volkano yake ni mojawapo ya chache duniani zinazolipuka na lava adimu ya ‘’carbonatite’’.
Mapema Septemba 2007, ililipuka na kusababisha kuwepo kwa wingu la majivu kwenye angahewa.
Milima ya kenya
Nchini Kenya Mlima Kenya, ina kilele kirefu cha pili barani Afrika kikiwa mita 5,199 na hii ni hazina nyingine ya Afrika Mashariki.
Mlima huu wa volkano iliyotyulia ulilipuka mara ya mwisho zaidi ya miaka milioni 2.6 iliyopita.
Kwenye mipaka ya Kenya na Uganda, kuna Mlima Elgon..Ni mojawapo ya milima mirefu zaidi barani ikiwa karibu mita 4,321. Inasemekana kuwa ililipuka mara ya mwisho zaidi ya miaka milioni 24 iliyopita.
Volkano za DRC
Milima mingine ya volkano iko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC).
Mlima Nyiragongo, mojawapo ya volkano zenye nguvu zaidi barani Afrika, uko DRC.
Shughuli inayoendelea na, haswa, ziwa la lava linalovutia hufanya hii kuwa volkano maarufu sana.
Volkano hiyo imeripotiwa kulipuka zaidi ya mara 35 na mlipuko mbaya zaidi ulitokea mnamo 1977, wakati zaidi ya watu 600 waliuawa.
Ya hivi punde ilikuwa mwaka wa 2021, wakati watu 32 walifariki kutokana na mlipuko huo na nyumba 1,000 ziliharibiwa.
Volkano nyingine nchini DRC ni Mlima Nyamuragira, unaopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Virunga.
Inaaminika kuwa moja ya volkano zenye nguvu zaidi barani Afrika. Inasemekana imelipuka zaidi ya mara 40 ikiwa ni pamoja na mwaka wa 2004, 2006,2008 na 2011.
Mlima huo wa Nyamuragira unajulikana kwa uzalishaji wake wa mara kwa mara wa mtiririko wa lava unaoenda kwa kasi, na kuufanya kuwa mojawapo ya chanzo cha volkano ambazo zinaweza kulipuka wakati wowote.
Kwenye mpaka kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuna Mlima Karisimbi, mlima wa 11 kwa urefu zaidi barani Afrika na kwa sasa volkano iko katika hatua tulivu.
Hizi ni baadhi tu ya Volkano za bara letu .











