Ndani ya tamaduni ya watu wa Jamii ya Samburu nchini Kenya, ni kigoda maalum kinachopewa heshima zake, kikiwakilisha nembo, mila na heshima ya jamii hiyo.
Hiki ni kati ya vitu vinavyoheshimika na vyenye thamani kubwa sana katika jamii yetu, hata mimi siwezi kukalia,” anasema Moreno Moreschi, mwakilishi wa vijana katika jamii ya Samburu.
Wale wanaokifahamu, wanakiita ‘kiti kidogo kitukufu’, na wale wasiokijua, vizuri, hawathubutu hata kukigusa.
"Tunaamini kuwa Mungu amewapa watu maalum pekee katika jamii yetu talanta ya kutengeneza kigoda hiki," anaeleza Loshelen Lolosoli, mzee wa rika katika jamii hiyo.
Hadi sasa, ni watu wachache wamepata kukikalia kigoda hicho. Wale walio bahatika, hawakudai tu heshima, lakini uwajibikaji ndani ya jamii hiyo.
Kwa kimo chake, kigoda hiki kina urefu wa inchi tano na umbo lenye mviringo kwa juu.
Kulingana na Mzee Lolosoli, vijana hawaruhusiwi kukalia kigoda hicho, kama ilivyo kwa wanawake.
Ila, wataruhusiwa tu kuwabebea waume zao kigoda hicho wakati wa sherehe tu, ndani ya jamii hiyo.
“Kigoda hiki kinatengenezwa na wazee peke yake na mimi ndiye mwenye kuhusika na utengenezaji wake,” anasema Meibekini Loldepe, Mzee mwenye miaka 60.
Kama ulikuwa hufahamu, ni marufuku kwa watoto wadogo kukikaribia kigoda hiko, kwani ni ‘kitukufu’ na chenye umuhimu wa kipekee ndani ya jamii hiyo.
Ikitokea, mwana jamii wa Samburu amevunja ama kuharibu kigoda hiko, basi jua atakabaliwa na faini kubwa.
“Kama ukiharibu au kuvunja kigoda hiki, utapaswa kuleta kondoo dume, tena mkubwa sana,” anasema Mzee Loldepe.
Kisha, wazee hujumuika pamoja na kula nyama ya kondoo huyo baada ya kuchinjwa.
Kigoda hiki, kina kazi nyingi.
Hutumika kuketia wakati wa mikusanyiko muhimu na wakati mwingine kama mto wa kupumzikia.
“Kwa sasa nina miaka 74, ila toka nimezaliwa nimekuta wanazingatia sheria na kanuni za kiti hiki,” anahitimisha Mzee Loldepe.