Mashambulizi ya kulipiza kisasa ya Iran mpaka sasa yamelenga maeneo 500 yanayohusishwa na Israel na Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, limesema Jeshi la Mapinduzi ikiwa ni siku ya tatu tangu kuanza kwa mapigano.
"Tangu kuanza kwa mapigano, wanajeshi jasiri wa vikosi vya Iran wameshambulia maeneo 60 ya kimkakati na maeneo 500 ya jeshi la Marekani na maeneo ya utawala wa Kizayuni (Israel)," limesema Jeshi hilo katika taarifa yake Jumatatu.
Vile vile limeongeza kusema kuwa limetuma ndege zisizo na rubani 700 na mamia ya makombora.
Iran imetumia makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani kujibu mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel ambayo yameanza Februari 28, na kumuua kiongozi mkuu wa dini Ali Khamenei na maeneo mengine.
Baadhi ya mashambulizi ya Iran yamelenga Israel moja kwa moja, na kusababisha vifo vya takriban watu 11 (pamoja na maeneo ya kati ya Israel kama Beit Shemesh na karibu na Jerusalem) huku kukiwa na majeraha kadhaa.
Iran pia imeshambulia kambi za Marekani katika eneo hilo, na kusababisha vifo vya takriban wanajeshi wanne wa Marekani na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Nchi za Ghuba zinazohodhi vikosi vya Marekani, kama vile UAE, Kuwait, Qatar, Bahrain, Saudi Arabia, na Oman, pia zimeshambuliwa moja kwa moja na makombora ya Iran pamoja na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwa jeshi, wananchi, pamoja na miundombinu.
Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) imesema Jumatatu kuwa wanajeshi 18 wa Marekani "wamejeruhiwa vibaya," tangu kuanza kwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, imeripoti CNN.
Taarifa hiyo ya msemaji Kapteni Tim Hawkins imefuatiwa na uthibitisho wa kifo cha nne, mwanajeshi ambae alifariki baada ya kujeruhiwa katika mashambulizi ya kwanza ya Iran.
Shambulizi baya zaidi ni lile lililotokea katika mji wa Minab kusini mashariki mwa Iran, ambalo liliua wanafunzi 180.









