Wakati taifa la Senegal likiwa bado kwenye shamrashamra za ubingwa wa AFCON, Brahim Diaz bado anatafakari ni kwa namna gani alishindwa kufunga ile penati dhidi ya Édouard Mendy, ambayo pengine tungekuwa tunaongea mengine kwa wakati huu.
Diaz, nyota wa Morocco anayeichezea Real Madrid ya nchini Hispania, alikosa kufunga tuta lile lililokuwa na utata, baada ya kuamua kupiga kwa mtindo wa Panenka.
Asili ya Panenka
Mwaka 1976, ndani ya dimba la Crvena Zvezda jijini Belgrade, kwenye iliyokuwa Yugoslavia ya wakati huo, ubao wa matokeo ulikuwa unasomeka 2-2.
Ilikuwa ni fainali ya EURO iliyowakutanisha Czechoslovakia dhidi ya Ujerumani Magharibi kwa wakati huo.
Timu hizo zikiwa zimetoka suluhu ndani ya muda wa kawaida, mbungi ilibidi iamuliwe kwa mikwaju ya penati, na baada ya Uli Hoeness kuangua mnazi kwa upande wa Ujerumani Magharibi, akajongea mwamba mmoja aitwaye Antonín Panenka, ambaye aliamua kuubetua mpira kiustadi au kuupiga beleshi, na kumpeleka marikiti golikipa wa Ujerumani Magharibi Sepp Maier.
Na huo ndio ukawa mwanzo wa mtindo huu wa upigaji penati.
Hata hivyo, mtindo huo umekuwa na majina tofauti kulingana na nchi.
Kwa mfano, ukienda Italia, mtindo huu huitwa cucchiaio ('yaani kijiko’).
Kwa wenye soka lao kule Brazil, wao huuita Cavadinha (yaani mchoto mdogo), wakati Argentina, hujulikana kama Picado.
Baadhi ya wachezaji maarufu waliowahi kufunga kwa mtindo huu ni pamoja na Andrea Pirlo, Zinedine Zidane, Alexis Sanchez, Sebastian Abreu na Francesco Totti.
Katika mchezo wa robo fainali ya Copa America kati ya Argentina na Ecuador uliofanyika Julai 4, 2024, Lionel Messi alikosa penati yake baada ya kujaribu kufunga kwa penati, mchoto wake ukiisha kulenga mtambaa wa panya.













