| Swahili
Kenya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama uliosimamisha mkataba wa biashara wa Umoja wa Ulaya
Shirika lisilo la kiserikali la Centre for Law Economics and Policy, liliwasilisha kesi hiyo dhidi ya Kenya kwa misingi kuwa makubaliano yalikiuka baadhi ya vipengele vya mkataba wa kuanzisha soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki
Kenya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama uliosimamisha mkataba wa biashara wa Umoja wa Ulaya
Kenya iliuza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 1.56 kwa EU mwaka jana / Public domain
1 Desemba 2025

Kenya inasema itakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya kikanda uliositisha mkataba wa kibiashara na Umoja wa Ulaya, Waziri wa Biashara Lee Kinyanjui alisema, akiongeza kwamba uamuzi huo unahatarisha biashara kati yao na EU ya dola bilioni 1.56 kwa mwaka.

Mahakama ya Afrika Mashariki yenye makao yake makuu mjini Arusha, Tanzania ilisitisha utekelezaji wa mkataba huo wiki iliyopita , Kinyanjui alisema, ili kusubiri matokeo ya kesi iliyowasilishwa na shirika lisilo la kiserikali linaloupinga.

Kenya ilitia saini mkataba huo, unaojulikana kama Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi, na Umoja wa Ulaya mwaka wa 2023 ili kuhakikisha upatikanaji wa soko la bidhaa katika jumuiya hiyo ya mataifa 27, na kuweka orodha ya bidhaa za Ulaya kufikia soko la Kenya baada ya muda.

Baadhi ya vipengele vya kesi ya kupinga makubaliano hayo kwenye tovuti ya mahakama hiyo vilionesha shirika lisilo la kiserikali la Centre for Law Economics and Policy, liliwasilisha kesi hiyo dhidi ya Kenya kwa misingi kuwa makubaliano na EU yalikiuka baadhi ya vipengele vya mkataba wa kuanzisha soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambalo Kenya ni mwanachama.

Sasa wizara ya biashara imeanzisha mchakato wa kukata rufaa ili kutupilia mbali agizo la mahakama, Kinyanjui alisema.

Waziri hakusema ni lini rufaa hiyo itasikilizwa na mahakama.

"Mkataba wa EPA wa Kenya-EU ndiyo tegemeo la mauzo yetu ya nje na uti wa mgongo wa maisha kwa Wakenya wengi," Kinyanjui alisema katika taarifa yake.

"Kenya itaendelea kufanya biashara na EU na hatua zinachukuliwa ili kuhakikisha uendelevu, mipango na kulinda misingi yetu ya kibiashara iliyopo."

Wakati Kenya iliuza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 1.56 kwa EU mwaka jana, taifa hilo liliagiza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 2.09 kutoka kwa umoja huo, waziri huyo alisema.

Mataifa ya Kiafrika yamekuwa yakitafuta kuongeza mauzo yao ya nje kwa masoko kama vile EU na China, baada ya kutozwa ushuru wa juu zaidi na serikali ya Marekani mwaka huu.

CHANZO:Reuters