Kwanini Afrika inatishiwa na 'utasa' licha ya kuwa na idadi inayokua zaidi duniani
AFRIKA
5 dk kusoma
Kwanini Afrika inatishiwa na 'utasa' licha ya kuwa na idadi inayokua zaidi dunianiMiongoni mwa changamoto kubwa za utasa ni kuwepo kwa shinikizo kutoka kwa jamii hasa kwa wanandoa.
Ugumba, si wanandoa pekee ndio wanaoathirika bali jamii nzima, kwa suala la unyanyapaa/ Reuters / Reuters
10 Desemba 2025

Miongoni mwa taarifa zilizovutia wasomaji wengi zaidi mitandaoni ni za Halima Cissé - mwanamke kutoka Mali - aliyejifungua watoto tisa mwezi Mei 2021.

Habari zake zilifuatiliwa kwa mshangao au hata matamanio kwani kwa Waafrika wengi, kupata mtoto ni baraka kubwa, bali kupata watoto wengi kiasi hiki kwa mpigo ni baraka zaidi. Jambo la kusheherekewa.

Na mara kwa mara utasikia baadhi ya familia za Kiafrika zinazopata watoto wengi, aidha ni kwa mama mmoja kujifungua au kutokana na ndoa za wake wengi.

Lakini licha ya taswira hii, kuna kilio cha siri kinachowaumiza wanandoa wengi, nacho ni utasa/ ugumba.

‘‘Kuna dhana kuwa Afrika haina tatizo la uzazi,’’ anasema Dkt Wanjiru Ndegwa Mshauri na
Mtaalamu wa Uzazi katika kituo cha Footsteps To Fertility Centre Nairobi, Kenya.

‘‘Nilihudhuria mkutano hivi majuzi na profesa mzima kutoka Ujerumani alipendekeza ufadhili usipotezwe katika masuala ya uzazi barani Afrika kwa sababu bara hili tayari lina watu wengi. Unaweza kufikiria nilivyoshtuka,’’ Dkt Wanjiru anaiambia TRT Afrika.

Kwa mujibu wa wataalamu, idadi ya raia katika nchi au bara, sio ishara tosha ya hali ya uzazi. Nchi inaweza kuwa na idadi kubwa ya raia lakini pia kunaweza kuwa na watu wengi wenye matatizo ya uzazi.

Shirika la Afya Duniani WHO linafafanua utasa au ugumba, kama kushindwa kupata ujauzito baada ya miezi 12 au zaidi ya kujamiiana bila kinga. Hii inaaminiwa kuathiri mtu 1 kati ya 6 wa umri wa kuzaa wakati fulani katika maisha yao.

"Ugumba ni mojawapo ya changamoto za afya ya umma ambazo hazizingatiwi sana wakati wetu na suala kuu la usawa duniani kote," alisema Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO. "Mamilioni wanakabiliwa na safari hii ya upweke - kwa kutengwa kutokana na gharama ya juu ya utunzaji, kusukumwa kuelekea matibabu ya bei nafuu ambayo ni hatari na hayajathibitishwa, au kulazimishwa kuchagua kati ya matumaini yao ya kupata watoto na usalama wao wa kifedha,’’ Dkt Tedros anaongeza.

Mwongozo wa kwanza wa WHO wa Utasa

Sasa WHO imetoa mwongozo wa kwanza wa kimataifa kuhusu utasa/ ugumba.

Shirika hilo linasema kuwa mwongozo huo wa mapendekezo 40 unalenga kuimarisha kinga, utambuzi na matibabu ya utasa. Inatoa chaguzi za gharama nafuu katika kila hatua, huku ikitetea ujumuishaji wa huduma ya uzazi katika mikakati ya kitaifa ya afya, huduma na ufadhili.

Wataalamu wanaona mwongozo huu umekuja wakati muafaka.

‘‘Tunakosa kila kitu kiukweli. Hatuna wataalamu wa kutosha wanaoelewa jinsi ya kuhudumia utasa. Hatuna vituo vya kutosha vya Upandikizaji wa mimba (IVF), hatuna wataalam wa maisha ya kiini tete (embroyolojia). Kwa kweli kwetu Kenya tunakosa wataalam wa embriolojia na hakuna taasisi zinazotoa mafunzo ya aina hiyo.’’

Chini ya mwongozo wa WHO, kuna mapendekezo ya hatua za udhibiti bora wa kliniki wa utasa. Pia inatoa wito wa kuongezeka kwa uwekezaji katika kuzuia, ikiwa ni pamoja na taarifa kuhusu uzazi na ugumba, mambo kama vile umri, huduma shuleni, huduma za afya ya msingi na vituo vya afya ya uzazi.

Unyanyapaa katika jamii

Miongoni mwa changamoto kubwa za utasa ni presha zinazotoka kwa jamii hasa kwa wanandoa.

Wanawake mara nyingi wanalaumiwa kwa kukosa kushika mimba katika ndoa jambo ambalo wataalamu wanakosoa kama unyanyapaa usio na uelewa wowote.

‘‘Kumbuka katika utasa, sio wanandoa pekee ndio wanaoathirika bali jamii nzima, kwa suala la unyanyapaa ambao wanandoa wanapitia,’’ Dkt Wanjiru anaambia TRT Afrika. ‘‘Hadi leo, hata kabla ya harusi, mwanamke anapewa shinikizo kubwa kwamba tunapenda digrii zako lakini sasa tunahitaji kukuza familia. Katika mazingira ya familia bado ni ngumu sana,’’ anaongeza.

Hata hivyo, Dkt Wanjiru anasema kuwa wameshuhudia ongezeko kubwa la wanaume wanaotafuta ushauri au hata tiba katika kliniki zao kuonyesha kuwa wanaume zaidi wanapata uelewa kuwa tatizo linaweza kutokea upande wao, au kuwa lazima wasuluhisho.

Chaguo la suluhisho

Mwongozo wa WHO unasisitiza haja ya kukabiliana na mambo ya hatari ya utasa, ikiwa ni pamoja na magonjwa ya zinaa yasiyotibiwa na matumizi ya tumbaku. mabadiliko katika mtindo wa maisha - kama vile lishe bora, mazoezi ya mwili, na kuacha utumiaji wa tumbaku - zinapendekezwa kwa watu binafsi na wanandoa wanaopanga au kujaribu ujauzito. Kuwafahamisha watu kuhusu uzazi na ugumba mapema kunaweza kuwasaidia katika kufanya mipango ya uzazi.

Lakini je kuna muda muafaka wa kuchunguza au kutafuta usaidizi kwa uzazi?

‘‘Nimekuwa na wanandoa ambao wamekuwa pamoja kwa mwezi mmoja na wanashangaa haikufanyika mwezi huu lakini haifanyiki kwa mwezi mmoja, tunahitaji angalau mwaka mmoja ili tujaribu na kuishi pamoja kabla hatujawa na wasiwasi. Lakini sidhani kuna haja ya kukimbilia uchunguzi wa mapema au kila mara,’’ anashauri Dkt Wanjiru.

Kwa kutambua athari ya kutokuwa na uwezo wa kupata uja uzito, ambayo inaweza kusababisha unyogovu, wasiwasi na hisia za kutengwa na jamii, mwongozo wa WHO unasisitiza haja ya kuhakikisha upatikanaji unaoendelea wa msaada wa kisaikolojia kwa wale wote walioathirika.

WHO inahimiza nchi kurekebisha sera zao za ndani na kufuatilia maendeleo. Utekelezaji wenye mafanikio utahitaji ushirikiano katika Wizara za Afya, jumuiya za wataalamu wa afya, jumuiya za kiraia na vikundi vya wagonjwa.

Kwa sasa wataalamu wanasema tiba zipo, suluhisho zipo ila inategemea kwa kiasi kikubwa sababu mahsusi kwa mtu au wanandoa kukosa uwezo wa kupata uja uzito.

‘‘Kuna suluhisho lakini suluhisho hazipatikani kwa urahisi au kukubalika kwa kila mtu. Inategemea sana sababu ya utasa wako ni nini,’’ anasema Dkt Wanjiru.

CHANZO:TRT Afrika Swahili