Kukamatwa kwa John Hiche kunakuja siku chache tu kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika Tanzania.
Aidha, chama kikuu cha upinzani CHADEMA kimekataa kushiriki katika uchaguzi huo, huku mgombea wa Urais wa chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, kuondolewa kwenye kinyang’anyiro na Tume Huru ya Uchaguzi ya Tanzania (INEC).
Kuelekea uchaguzi huo, wanasiasa wa upinzani pamoja na makundi ya haki za binadamu wameishtumu serikali kwa vitendo vya utekaji nyara na kukamatwa kwa wapinzani wa kisiasa.
Rais Samia Hassan amesema kuwa serikali yake imejizatiti kuheshimu haki za binadamu na aliagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu ripoti za utekaji nyara mwaka jana. Hata hivyo, matokeo rasmi ya uchunguzi huo hayajawahi kutolewa hadharani.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, alikuwa anazuiliwa katika kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam, mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, kama alivyoeleza Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, kwa waandishi wa habari, akiongeza kuwa maafisa hawakutoa sababu yoyote ya kumkamata.
Heche alikamatwa nje ya Mahakama Kuu ya jiji hilo alipokuwa amewasili kuhudhuria kesi ya kiongozi wa chama hicho, Tundu Lissu, kwa mujibu wa msemaji wa chama, Brenda Rupia, aliyeandika kupitia mtandao wa kijamii wa X.
Alisema polisi hawakuwa wametoa sababu ya kumkamata na walimhamishia Tarime, kaskazini-magharibi mwa Tanzania, bila kutoa maelezo zaidi.
Hayo yakijiri, Idara ya Uhamiaji ilisema katika taarifa yake Jumamosi kuwa Heche aliondoka nchini bila kufuata taratibu. Chama chake kilikanusha madai hayo, kikisema kuwa alikuwa anatarajiwa kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga.
Hadi sasa, msemaji wa serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, hakutoa ufafanuzi wowote kuhusu kukamatwa kwa Heche siku ya Jumatano.