Mahakama ya Tunisia imewaachilia kundi la wafanyakazi wa misaada baada ya kuwapa vifungo vya nje kwa kosa la kuwezesha 'kuingia na kukaa bila vibali' kwa wahamiaji, ilisema kamati ya msaada siku ya Jumanne.
Sherifa Riahi, mkurugenzi wa zamani wa Shirika lisilokuwa la serikali la Terre d'Asile, na baadhi ya wafanyakazi wake walikuwa tayari wamekaa gerezani kwa zaidi ya miezi 20 kabla ya kusikilizwa kwa kesi yao Jumatatu.
Saa chache baada ya kusikilizwa, kamati ya msaada ya Riahi ilitoa video ikimuonyesha akiondoka gerezani usiku na kutangaza kuwa wenzake pia wameachiliwa.
Mahmoud Daoud Yaacoub, mmoja wa mawakili wa upande wa utetezi wa Riahi, aliiwaambia waandishi kuwa mahakama ilitoa hukumu hiyo ya kusimamishwa kwa miaka miwili kwa watuhumiwa waliokuwepo kizuizini kabla ya kesi.
Mashtaka mengine yalifutwa
"Kesho tutaelewa hukumu iliyosalia kuhusu watuhumiwa waliotolewa kwa dhamana," alisema.
Wafanyakazi wa NGO walituhumiwa pamoja na wafanyakazi wengine 17 wa manispaa kutoka mji wa mashariki wa Sousse ambao walihusishwa kwa kukodisha majengo kwa shirika.
Watuhumiwa 23, ambao pia walishtakiwa kwa 'kufanya njama kwa lengo la kuwahifadhi au kuwaficha watu walioingia kwa njia haramu nchini', walikabiliwa na adhabu ya hadi miaka 10 gerezani.
Mashtaka mengine, yakiwemo yale yaliyodai uhalifu wa kifedha, yalitupiliwa mbali hapo awali.
Mawakili wa watuhumiwa walisema walikuwa wakitekeleza jukumu lao kwa misingi ya ubinadamu chini ya mpango uliokubaliwa na serikali, kwa uratibu na mamlaka.
Kituo muhimu cha mpito
Siku ya mwisho ya kesi Jumatatu, watu wachache walikusanyika nje ya mahakama kuunga mkono watuhumiwa. Kusikilizwa kwa mwisho kulidumu siku nzima na usiku ulipofika, mahakama ilikaa faragha ili kutoa hukumu.
Mkurugenzi maalum wa UN wa walinda haki za binadamu, Mary Lawlor, siku ya Jumapili alitoa wito" kwa mamlaka wamwachilie yeye (Riahi) badala ya kumshtaki kwa mashtaka ya kuibua shaka yanayohusiana na utetezi wake wa haki za wahamiaji."
Uhamiaji ni suala nyeti nchini Tunisia, ambayo ni kituo muhimu cha mpito kwa maelfu ya watu wanaojaribu kufika Ulaya kila mwaka.
Watuhumiwa walikamatwa Mei 2024 pamoja na takriban wafanyakazi kumi na wawili wa mashirika ya misaada.





















