Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amewataka vijana kukataa kutumika kwa maslahi ya wengine wenye nia ovu, huku akiwahakikishia wananchi kuwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 unafanyika kwa amani na salama.
Kulingana na Wasira, yapo baadhi ya mashirika ya kimataifa yanatamani kuona amani iliyopo nchini humo inavurugika, akiwahahakishia kuwa chama hicho kimesimama imara kulinda amani, umoja na mshikamano wa Watanzania.
"Nataka niwaambie Watanzania uchaguzi utafanyika tarehe 29 tena kwa amani, na yule ambaye anaota amani itapotea anapoteza wakati wake, kwa sababu CCM bado tunashikilia dola, amani itakuwa tele, waambieni wapigakura hakuna mtu atakayefanya chochote,” alisema Wasira.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, alibainisha kuwa yapo baadhi ya mashirika ya kimataifa yasiyotaka kuona amani inaendelea kuwepo nchini humo na kuwa yapo tayari kutoa fedha kuvuruga utulivu wa Watanzania.
"Yapo baadhi ya mashirika ya kimataifa yana matatizo na mengine hayataki kuona amani ya nchi yetu, yapo tayari kutoa fedha ili amani itoweke," ameeleza.
Aidha, Wasira amewataka vijana wakatae kutumika kuleta vurugu kwa kuwa ustawi wa maendeleo yao na nchi kwa ujumla unategemea amani na utulivu.