Kenya kuanza kufuatilia taasisi za umma zisizotoa vituo vya malezi kwa wazazi wenye watoto wadogo
AFRIKA
5 dk kusoma
Kenya kuanza kufuatilia taasisi za umma zisizotoa vituo vya malezi kwa wazazi wenye watoto wadogoKwa mujibu wa taarifa za serikali, sehemu nyingi za kazi za umma - ikiwa ni pamoja na taasisi za elimu na ofisi za utumishi wa umma - zimechelewa katika kutenga maeneo salama na ya kuaminika ya malezi ya watoto, licha ya mfumo uliopo wa kisheria
ILO inapendekeza kutengwa vituo vya malezi katika lsehemu za kazi / Picha ILO / others
12 Januari 2026

Kenya inatazamiwa kuanza msako wa kitaifa Januari 2026 dhidi ya taasisi za umma ambazo zimeshindwa kutekeleza sheria inayohitaji kuanzishwa kwa vituo vya kulelea watoto (“creche”) kwa wafanyikazi wa kike.

Agizo hili la utekelezaji linatoka kwa Wizara ya Afya, huku maafisa wakisisitiza kwamba hitaji la kisheria si la hiari na ni lazima litekelezwe ili kuwalinda akina mama wanaofanya kazi na watoto wao.

Japo linaonekana kuchelewa, wazazi wengi wamelipongeza kuwa litasaidia hasa akina mama walio na changa moto ya kukosa mtu wa kumuachia watoto wanapokwenda kazini.

‘‘Nakumbuka vijana wangu wote wawili niliwanyonyesha kikamilifu miezi sita ya kwanza,’’ anakumbuka Fridah Archie, mzazi nchini Kenya. ‘‘ Nililazimika kutafuta sehemu ya kukamua maziwa kwenye chupa kila baada ya saa chache, huku kazi inanisubiri. Ilikuwa ngumu sana. Ningekua na sehemu hapo kazini mtoto wangu anaweza kuangaliwa ingekuwa rahisi zaidi.’’ Fridah anaambia TRT Afrika.

Wengi wanachukulia sheria kwa wepesi

Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, sehemu nyingi za kazi za umma - ikiwa ni pamoja na taasisi za elimu na ofisi za utumishi wa umma - zimechelewa katika kutenga maeneo salama na ya kuaminika ya malezi ya watoto, licha ya mfumo uliopo wa kisheria unaowalazimisha waajiri kutoa msaada huo.

Utekelezaji duni umeripotiwa kuvuruga utendakazi na kuchangia mfadhaiko na usumbufu miongoni mwa akina mama wanaofanya kazi ambao wanatatizika kusawazisha majukumu ya malezi na kazi.

Katibu Mkuu wa wizara ya Afya ya Umma, Mary Muthoni, amesema taasisi nyingi zimeichukulia sheria kwa wepesi , na kuonya kwamba utekelezaji utaanza Januari ili kuonyesha kwamba sheria hiyo ina uzito kamili wa kikatiba.

"Wazo hilo sio sahihi. Sheria hii si ya hiari. Kuanzia Januari, tutaitekeleza kikamilifu ili kuwalinda akina mama wanaofanya kazi na watoto wao," alisema Muthoni.

Vituo vya malezi vinasaidia kupunguza ‘utoro’

Takwimu kutoka tafiti mbali mbali zilizofanywa na Shirika la Wafanyakazi ILO, na shirika la Fedha IFC, zinaonyesha ukosefu wa malezi ya watoto yenye muundo huathiri kwa kiasi kikubwa ushiriki wa wanawake katika nguvu kazi na ustawi wao.

Wanawake hupewa mgao usio na uwiano wa malezi ya watoto, mara nyingi hutumia saa nyingi zaidi kwenye kazi ya matunzo isiyolipwa kuliko wanaume, jambo ambalo linapunguza uwezo wao wa kutafuta ajira ya kulipwa, elimu, na maendeleo ya kazi.

Tafiti hizi pia zinaonyesha kuwa upatikanaji wa vifaa vya kutunza watoto mahali pa kazi, kama vile vyumba vya kunyonyesha na vituo vya malezi, unahusishwa na viwango vya juu vya unyonyeshaji wa kipekee na uendelevu wa ajira kwa mama wachanga.

Kutokuwepo kwa huduma za malezi ya watoto kunaweza kusababisha utoro, kupungua kwa tija, na kupunguka kwa kazi huku akina mama wakitatiza malezi ya watoto wachanga na mahitaji ya kazi, na hivyo kuimarisha vizuizi vya kijinsia katika ajira.

Sheria ni ya wote

‘‘Naomba kama serikali ingefuatilia utekelezaji wa sera hii hadi kwa ofisi zisizo za serikali. kwasababu mimi binafsi sijawahi kuajiriwa katika ofisi ya serikali, na matatizo ni hayo hayo pia japo wakati mwingine hata ni mbaya zaidi kwa wazazi wachanga,’’ Fridah anaambia TRT Afrika.

Lakini Katibu Mkuu Mary Muthoni amefafanua kuwa sheria hii ni ya wote.

‘‘Kila kampuni, kila eneo la utumishi, kila taasisi katika nchi hii lazima wajenge eneo la malezi ya watoto. Na hili silo agizo langu tu, sheria ndivyo inavyosema. Sheria ya Afya ya mwaka 2017 inaagiza kuwa kila taasisi lazima iwe na kituo cha malezi.’’ anasema Muthoni.

Katika kanda ya Afrika Mashariki, sera zinazoangazia malezi ya watoto mahali pa kazi zinatofautiana, na huduma ya lazima ya watoto inayotolewa na mwajiri bado ni nadra:

Hali katika Kanda ya Afrika Mashariki

Nchini Uganda, juhudi za kisheria kama vile Mswada wa (Marekebisho) ya Ajira wa 2022 ni pamoja na mahitaji yaliyopendekezwa kwa waajiri kutoa huduma za kulelea watoto na kunyonyesha, lakini utekelezaji unasubiri idhini ya rais na usambaaji katika sekta mbali mbali, na wanawake wengi hufanya kazi katika mazingira yasiyo rasmi ambapo sheria hizi hazitumiki sana.

Sheria za kazi za Tanzania zinaongeza ulinzi wa haki za mama na baba lakini haziamuru kwa uwazi huduma za malezi ya watoto mahali pa kazi. Hata hivyo sheria imewaruhusu kina mama waliorudi kutoka likizo ya kujifungua muda wa saa mbili kuwanyonyesha watoto wao ambapo wataamua wenyewe wakati wa kutumia muda huo.

Rwanda imeongeza vituo vya ECD (malezi ya utotoni) mahali pa kazi na "vyumba vya akina mama" vikianzishwa katika baadhi ya taasisi, lakini hivi vinaendeshwa na programu za kibinafsi za kampuni na miradi ya mashirika kuliko mahitaji ya lazima ya kisheria.

Uchambuzi wa sheria za malezi ya watoto katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwa ni pamoja na Afrika Mashariki, unapendekeza hakuna nchi bado inawaamuru waajiri kujenga au kuendesha vituo vya kulelea watoto katika sehemu zote za kazi - na inafanya utekelezaji wa Kenya kujitokeza katika kanda, hata kama mifumo ya kisheria bado inatofautiana.

Huku Kenya ikianza kampeni ya kufuatilia utekelezaji wa sera hii kuanzia Januari, wengi wanatazamia kama kuweka kielelezo cha utekelezaji thabiti wa sera za mahali pa kazi zinazozingatia jinsia katika kanda na kuashiria kwamba nia ya kisheria ya kusaidia akina mama wanaofanya kazi lazima ioanishwe na miundombinu inayoonekana ya mahali pa kazi na ufuatiliaji.

CHANZO:TRT Afrika Swahili