Jeshi la Marekani limeandaa mipango mipya ya mashambulizi inayojumuisha uwezekano wa kutumia bomu lake kubwa zaidi lisilo la nyuklia (GBU-43/B, MOAB) dhidi ya miundombinu ya nishati na vituo vya nyuklia vya Iran, iwapo Rais Donald Trump ataamuru kuanzishwa upya kwa operesheni hiyo. .
Kwa mujibu wa taarifa ya CNN ya Jumatano, ikinukuu maafisa kadhaa wa Marekani wanaofahamu mipango hiyo, ni kwamba matumizi ya bomu hilo yanaweza kuashiria ongezeko kubwa la mashambulizi katika mzozo kati ya Marekani na Iran.
Hata hivyo, baadhi ya maafisa wameibua mashaka kuhusu uwezo wa bomu hilo kufanikisha malengo ya kijeshi ya Marekani, hasa katika kuharibu vituo vya nyuklia vilivyojengwa chini kabisa ya ardhi.
Kwa mujibu wa CNN, Trump ameielekeza jeshi kuandaa njia mbadala za kutekeleza mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, yakiwemo miundombinu ya nishati na vituo vinavyohusishwa na mpango wa nyuklia wa nchi hiyo.
Mipango hiyo inaweza kutekelezwa kabla au baada ya uchaguzi wa nusu muhula nchini Marekani.
Chanzo kimoja kinachofahamu mipango hiyo kiliiambia CNN kuwa mashambulizi yanaweza kufanyika kabla ya majeshi ya Marekani kujiondoa katika eneo la operesheni linalosimamiwa na Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM). Hali hiyo inaweza kuipa serikali ya Trump nafasi ya kufanya mashambulizi zaidi kabla ya kutangaza ushindi na kuondoa vikosi vyake.
Chanzo kingine kilisema kuwa mipango ya kushambulia maeneo ya nyuklia ya Iran inajumuisha wazi uwezekano wa kutumia MOAB, ikiwemo dhidi ya kituo kinachoshukiwa kuwa chini ya ardhi katika eneo la Mlima Pickaxe.
Trump amekuwa akitishia mara kadhaa kushambulia eneo hilo lililopo katika mkoa wa Isfahan. Marekani na Israel zinaamini kuwa Iran imehifadhi baadhi ya vifaa vinavyohusiana na mpango wake wa nyuklia katika eneo hilo.
Trump amesisitiza kuwa kuizuia Iran kupata silaha ya nyuklia ni mojawapo ya malengo makuu ya operesheni za kijeshi za Marekani dhidi ya nchi hiyo.
Mashaka kuhusu ufanisi wa bomu hilo
Afisa mmoja wa Marekani aliiambia CNN kuwa wanaopanga mipango ya kijeshi huandaa mara kwa mara njia mbadala za operesheni kwa ajili ya viongozi wa nchi, kuanzia mashambulizi ya kiwango cha chini hadi mashambulizi makubwa dhidi ya malengo yenye ulinzi imara.
Hata hivyo, bado kuna mashaka kuhusu uwezo wa MOAB kuharibu vituo vya nyuklia vilivyojengwa chini kabisa ya ardhi.
Bomu hilo linaloongozwa kwa kutumia mfumo wa ‘GPS’ lina uwezo wa kusababisha uharibifu mkubwa katika eneo la juu ya ardhi linalokadiriwa kuwa sawa na takribani mitaa tisa ya jiji. Hata hivyo, halijatengenezwa mahsusi kwa ajili ya kupenya kwenye tabaka nene za ardhi na kufikia malengo yaliyo chini sana ya ardhi.
Vyanzo vilivyonukuliwa na CNN vilisema kuwa huenda bomu hilo likashindwa kuharibu vituo vilivyolindwa na tabaka nene za miamba ya ‘granite’ pamoja na mifumo mingine imara ya ulinzi.
Chanzo kimoja kinachofahamu majadiliano kuhusu mipango hiyo kiliiambia CNN kuwa MOAB ni silaha kubwa inayofaa zaidi kwa kusababisha uharibifu katika eneo pana, lakini si chaguo linalofaa kwa malengo yanayohitaji kupenya ndani kabisa ya ardhi.
Iwapo litatumika, bomu hilo linaweza kusababisha uharibifu mkubwa katika eneo litakalolengwa. Wigo wake mpana wa mlipuko unaweza pia kuongeza hatari ya vifo na majeruhi miongoni mwa raia, hasa iwapo miundombinu ya nishati iliyo karibu na makazi ya watu au maeneo mengine ya kiraia italengwa.
MOAB lilitumika mara moja pekee katika mapigano, mwaka 2017, lilipodondoshwa dhidi ya maficho ya kundi la kigaidi la Daesh yaliyokuwa katika mfumo wa mapango katika mkoa wa Nangarhar, nchini Afghanistan.
Shinikizo la kisaikolojia
Licha ya mapungufu yake, maafisa wa Marekani wanaripotiwa kutathmini pia athari za kisaikolojia zinazoweza kusababishwa na matumizi ya bomu hilo, kama sehemu ya chaguo pana za kijeshi zinazozingatiwa na serikali ya Trump.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja kilichozungumza na CNN, Trump anaweza kukabiliwa na shinikizo la kuchukua hatua zaidi dhidi ya Iran, licha ya kutokuwa na uhakika iwapo mashambulizi ya ziada yatailazimisha Iran kukubali matakwa ya Marekani.
Chanzo hicho kilidokeza kuwa MOAB linaweza kutumiwa kama njia ya kuweka shinikizo la kisaikolojia kwa Iran, hasa kutokana na changamoto za kutumia silaha zilizopo kushambulia vifaa vilivyofichwa chini kabisa ya ardhi.

















