Clement Mzize: Mtanzania wa kwanza kutwaa kiatu cha dhahabu CAF
Clement Mzize akionesha tuzo yake mbele ya Watanzania./Picha:@CAFCLCC
Clement Mzize: Mtanzania wa kwanza kutwaa kiatu cha dhahabu CAF
Novemba 19, 2025, mshambuliaji wa Young Africans Sports ya nchini Tanzania, Clement Mzize alitunukiwa tuzo ya Goli Bora la 2025 tuzo iliyotolewa na shirikisho la Michezo barani Afrika CAF.
24 Novemba 2025

Anaitwa Clement Francis Mzize, kijana kutoka wilaya ya Muheza mkoani Tanga nchini Tanzania, aliyewainua mashabiki wa Young Africans na Watanzania wote, baada ya kombora lake dhidi ya TP Mazembe, kuchaguliwa kuwa goli bora la mwaka kwenye usiku wa tuzo za CAF zilifofanyika jijini Rabat nchini Morocco, Novemba 19.

Mzize aliachia shuti hilo kutoka umbali wa mita 30, katika mchezo wa hatua ya mtoano ya Kombe la Ligi ya Mabingwa wa Afrika, dhidi ya TP Mazembe ya DRC, ambapo Young Africans ilishinda kwa jumla ya mabao 3-1,  mwezi Januari mwaka huu.

Licha ya kutokuwepo kwenye usiku wa tuzo hizo ambazo zilitawaliwa na jina la Mmorocco Achraf Hakimi, bado mshambuliaji huyu wa kati kutoka mitaa ya Jangwani, alituma ujumbe wa shukrani kwa mashabiki wake.

Havumi ila yumo

Anaweza akawa hatajwi sana, lakini Clement Mzize ametokea kuwa mchezaji muhimu kwa klabu yake ya Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’.

Mara kwa mara, magoli yake muhimu na assists zake zimezipa matokeo Young Africans na Taifa Stars, kwenye michezo mbalimbali, hasa ile ya kimataifa.

Akiwa amezaliwa Januari 7, 2004 huko Muheza mkoani Tanga, Mzize alikulia katika mazingira ya kawaida tu.

 

Hata hivyo, alianza kuonesha mapenzi kwenye mchezo wa soka kupitia michezo ya mtaani na kushiriki mashindano ya shule.

Je, unafahamu kuwa ili aweze kupeleka mkono kinywani kabla ya kusajiliwa na timu kubwa, Clement Mzize alikwua dereva bodaboda?

Ndio. Shughuli hii ilimsaidia kuendesha maisha yake huku akiendelea kuonesha kipaji chake cha soka katika mashindano ya mtaani na ya vijana.

Mzize alianza kumulikwa na rada za klabu kubwa nchini Tanzania, hasa baada ya kung’ara katika mashindano ya vijana.

Moja kwa moja, alijiunga na Young Africans akianzia na kikosi cha Under 20, ambako aliwasha moto kweli kweli.

Msimu wa 2022-2023, Profesa Nasreddine Nabi, alimpandisha Mzize kwenye timu ya wakubwa, na hapo ndipo nyota yake ilipoendelea kung’aa.

Hata baada ya kuondoka Nabi na kuwasili kwa Gamondi, Mzize mwenye kimo cha mita 1.83, alikuwa na mwendelezo ule ule uwanjani, japo watu walimchukulia kama mchezaji wa kawaida tu.

Leo hii kijana huyo kutoka karibu na misitu ya Amani huko Tanga, anakuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa tuzo hiyo kubwa kwenye ngazi ya CAF.

Pia, anakuwa mchezaji wa pili wa Ligi ya NBC nchini Tanzania kufanya hivyo, baada ya aliyekuwa mchezaji wa zamani wa Simba Sports Club, Msenegali Pape Ousmane Sakho, kufanya hivyo mwaka 2022.

CHANZO:TRT Afrika Swahili