AFRIKA
2 dk kusoma
Uwanja wa ndege wa Khartoum, Sudan, wapokea ndege ya kwanza ya baada ya zaidi ya miaka miwili
Ndege ya abiria ya kampuni ya Badr Airlines imetua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum kwa mara ya kwanza tangu Aprili 2023, ikiwa ni ishara ya kurejea kwa safari za ndege za kiraia baada ya zaidi ya miaka miwili ya kufungwa.
Uwanja wa ndege wa Khartoum, Sudan, wapokea ndege ya kwanza ya baada ya zaidi ya miaka miwili
Uwanja wa ndege ulikuwa umefungwa kwa siku 921 tangu mapigano yalipozuka kati ya jeshi la serikali na RSF mnamo Aprili 2023. / / AA
tokea masaa 3

Uwanja huo wa ndege umepokea ndege yake ya kwanza ya abiria siku ya Jumatano, baada ya kufungwa kwa zaidi ya miaka miwili na nusu, kwa mujibu wa mamlaka za Sudan.

“Tuna furaha kutangaza kuwa ndege ya kampuni ya Badr Airlines imetua muda mfupi uliopita katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum, ikimaanisha kufunguliwa tena kwa uwanja huu na kurejea taratibu kwa shughuli za anga kutoka mji mkuu baada ya kusimamishwa kwa muda mrefu,” ilisema taarifa ya mamlaka ya uwanja wa ndege iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Mamlaka hiyo imeeleza kuwa kufunguliwa kwa uwanja huo ni “hatua muhimu kuelekea kuimarika kwa sekta ya usafiri wa anga ya Sudan na kurejea polepole kwa safari za ndege.”

Ufunguzi huu umetokea saa chache baada ya ulinzi wa anga wa Sudan kuzuia shambulio la droni lililofanywa na kikundi cha wanamgambo cha RSF mapema Jumatano, ikiwa ni shambulio la pili ndani ya saa 24.

Uwanja wa ndege ulikuwa umefungwa kwa siku 921 tangu mapigano yalipozuka kati ya jeshi la serikali na RSF mnamo Aprili 2023.

Usiku wa Jumatatu, Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Sudan ilitangaza kuwa uwanja huo ungefunguliwa tena Jumatano. Hata hivyo, shambulio la droni karibu na uwanja huo lilizua hofu mpya kuhusu usalama.

Kufungwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum, ambao ni kitovu muhimu cha usafiri wa anga katikati ya Sudan, kulisababisha kusimama kwa kiasi kikubwa kwa safari nyingi za ndege nchini humo.

Jeshi la Sudan na RSF wamekuwa wakipigana tangu Aprili 2023, vita ambavyo vimesababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000 na kuwafanya wengine milioni 14 kuyahama makazi yao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa na mamlaka za ndani.

Hata hivyo, tafiti kutoka vyuo vikuu vya Marekani zinakadiria kuwa idadi ya waliouawa huenda imefikia takriban 130,000.

CHANZO:AA