| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Iran yakanusha kuzungumza na Marekani baada ya Trump kudai kuwepo kwa “mazungumzo yenye tija"
Iran ilitoa onyo kali kwamba “itaharibu kabisa” miundombinu muhimu katika eneo lote la Mashariki ya Kati iwapo Marekani itatekeleza tishio la Trump la “kuangamiza” mitambo ya umeme ya Iran.
Iran yakanusha kuzungumza na Marekani baada ya Trump kudai kuwepo kwa “mazungumzo yenye tija"
Wizara ya mambo ya nje ya Iran ilieleza kuwa kauli za Trump ni njama ya kushusha bei za nishati. / Reuters
tokea masaa 7

Serikali ya Iran imekanusha vikali kuwepo kwa mazungumzo yoyote na Marekani, ikipingana na kauli za Rais wa Marekani Donald Trump aliyedai kuwa hivi karibuni kulikuwa na “mazungumzo yenye tija” kati ya pande hizo mbili.

Wizara ya mambo ya nje ya Iran, ilisema siku ya Jumatatu ya kwamba hakuna mazungumzo yanayoendelea kati ya Iran na Marekani. Wizara hiyo ilieleza kuwa kauli za Trump ni njama ya kushusha bei za nishati na njama ya kupata muda wa ziada kwa ajili ya kutekeleza mipango ya kijeshi, kwa mujibu wa chombo cha habari nchini Iran.

“Hamna mazungumzo kati ya Iran na Marekani,” liliripoti shirika la habari la Mehr, likinukuu wizara hiyo, huku likiongeza kuwa kauli za Trump ni sehemu ya juhudi za “kupunguza bei za nishati”.

Hata hivyo, Iran ilikiri kuwa baadhi ya nchi za kanda hiyo zimependekeza juhudi za kidiplomasia ili kupunguza mvutano uliopo.

“Sisi hatukuanzisha vita hivi, na matakwa kama hayo yanapaswa kuelekezwa Marekani,” iliongeza.

Katika muktadha wa mvutano huo, Tehran imekuwa ikijibu mashambulizi dhidi yake kwa kutumia droni na makombora dhidi ya majirani zake wa Ghuba. Mashambulizi hayo yamesababisha vifo, uharibifu wa miundombinu, pamoja na kuvuruga masoko ya kimataifa na usafiri wa anga, hasa pale miundombinu yake inaposhambuliwa na Marekani na Israel.

Mnamo tarehe 19 Machi, hatua ya kulipiza kisasi ya Iran baada ya Israel kushambulia uwanja wake muhimu wa gesi, ilisababisha kupungua kwa asilimia 17 ya uwezo wa Qatar wa kusafirisha nje gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG), na kusababisha hasara inayokadiriwa kufikia dola bilioni 20 kwa mapato ya mwaka.

Aidha, Irani ilionya kuwa “itaharibu kabisa” miundombinu nyeti katika Mashariki ya Kati, ikiwemo mifumo muhimu ya maji, ikiwa Marekani itatekeleza tishio la Trump la kuangamiza mitambo ya umeme ya Iran, iwapo Mlango wa Hormuz hautafunguliwa kikamilifu ndani ya siku mbili.

Awali, Trump alisema ameagiza kusitishwa kwa muda wa siku tano kwa mashambulizi yote dhidi ya mitambo ya umeme na miundombinu ya nishati ya Iran, akieleza kuwa hatua hiyo inatokana na kuwepo kwa “mazungumzo mazuri na yenye tija” na Tehran katika siku mbili zilizopita.

“Ninafuraha kuripoti kuwa Marekani na Iran zimekuwa na mazungumzo mazuri sana na yenye tija katika siku mbili zilizopita, kuhusu kufikia suluhisho la kudumu na kamili la uhasama wetu katika Mashariki ya Kati,” alisema Trump kupitia jukwaa lake la kijamii la Truth Social.

CHANZO:AA