Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Mlango Bahari wa Hormuz uko wazi, lakini meli zinahofia kuvuka kwa sababu ya vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
"Mlango Bahari wa Hormuz haujafungwa. Meli zinasitasita kwa sababu watoa bima wanaogopa vita ambavyo Israel ilianzisha- sio Iran," Abbas Araghchi alisema Jumapili kupitia ukurasa wa X.
"Hakuna mtoa bima - na hakuna raia wa Iran - atakayeyumbishwa na vitisho zaidi. Jaribuni kuwa na heshima," aliongeza.
"Uhuru wa kupita kwa meli hauwezi kuwepo bila uhuru wa biashara. Heshimu zote mbili - au usitegemee chochote."
Katika taarifa iliyotolewa kupitia mtandao wa X, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia ilisema Mlango-Bahari wa Hormuz "haujazuiwa."
Hata hivyo, imeongeza kuwa meli hizo "zinazomilikiwa na pande zinazofanya uvamizi haziwezi kuitumia kama njia za kawaida, na zitashughulikiwa kwa mujibu wa mfumo wa kisheria unaotokana na mzozo huo, pamoja na maamuzi na hatua za mamlaka husika ya Iran."
Tangu mwanzoni mwa mwezi Machi, Iran imefunga Mlango-Bahari wa Hormuz, njia kuu ya kupitisha mafuta ambayo kwa kawaida husafirisha mapipa milioni 20 kwa siku na takriban asilimia 20 ya biashara ya gesi asilia duniani, kwa meli nyingi.
Kufungwa kwa Hormuz kumeongeza gharama za usafirishaji na gharama ya bima kuongezeka, hivyo kuathiri bei ya mafuta, na kuibua wasiwasi wa kiuchumi wa kimataifa.
Siku ya Jumamosi, Rais wa Marekani Donald Trump alitishia "kuharibu" vinu vya umeme vya Iran, kuanzia na kubwa zaidi, ikiwa Iran haitafungua njia ya kimkakati ndani ya saa 48.
Uhasama katika eneo hilo umeongezeka tangu mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kuanza Februari 28, huku Tehran ikijibu kwa mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani na makombora yakilenga Israel na nchi za Ghuba zinazohifadhi mali za kijeshi za Marekani.
















