Usiku wangu katika kijiji cha wanawake nchini Kenya
MAISHA
4 dk kusoma
Usiku wangu katika kijiji cha wanawake nchini KenyaBaadhi ya wanawake hawa, waliwahi kupitia manyanyaso ya kijinsia ikiwemo kupigwa au hata kufukuzwa wakiwa na waume zao.
Kijiji cha wanawake nchini Kenya ni kimbilio la wanawake waliopitia unyanyasaji wa kijinsia. / TRT Afrika Swahili
13 Januari 2026

Katika Kaunti ya Samburu, kaskazini mwa Kenya, kuna kijiji kinachoongozwa na sheria moja kuu: wanaume hawaruhusiwi kuishi wala kulala hapa.

Kwa zaidi ya miongo mitatu, kijiji cha Ltungai kimekuwa mfano wa kijiji cha wanawake pekee.

Wanawake walioko hapa ni akina mama, mabinti, na watoto wao. Hakuna mwanamume hata mmoja.

Baadhi ya wanawake hawa, waliwahi kupitia manyanyaso ya kijinsia ikiwemo kupigwa au hata kufukuzwa wakiwa na waume zao.

Wengine walishambuliwa na kubakwa walipokuwa wakichunga mifugo yao kama mbuzi na ng’ombe, au hata walipokuwa wakikusanya kuni.

“Hiki ni kijiji chetu kama wanawake,” mkazi mmoja anamwambia mwandishi wa makala hii, na kuongeza, “Hakuna mwanamume anayeruhusiwa kulala hapa. Hakuna mwanamume anayeishi hapa.”

Wengi wao walijikuta wameishia katika makazi haya, badala ya kupata msaada au kuhurumiwa kwa yale waliyopitia, ikiwemo kulaumiwa au kutengwa na jamii.

“Wakati mambo haya yanapotokea,” anaeleza Pauline Loldepe, Kiongozi na Mratibu wa Wanawake kijijini humo, “Wanasema sisi tulikuwa wazembe, wanatuona kama watu wasio na maana katika jamii. Ndiyo maana tulikuja hapa.”

Leo hii, kuna jumla ya wanawake 38 ambao wanaishi pamoja na watoto wao katika kijiji hicho, wote wanategemeana kwa usalama wao.

Kijiji kilivyojengwa

Kijiji hiki kilianza kama hifadhi na kimbilio la wanawake hawa, na pole pole kilibadilika na kuwa kijiji kamili.

Kwa umoja na ushirikiano wao, wanawake hawa wamefanikiwa kujenga nyumba nne aina ya manyatta ambazo zinatumika kuwapa hifadhi wakazi wa kijiji hicho.

Manyatta ni makazi ya kitamaduni ya jamii ya Wasamburu; manyatta moja huwa na takribani nyumba ndogo sita zilizojengwa katika eneo moja.

Wanaume ambao ni baba wa watoto wanaoishi na wanawake hawa wanaruhusiwa kuwatembelea watoto wao, lakini nje ya mipaka ya kijiji.

Mwanamke anaweza kuondoka kijijini ili kupata ujauzito na baadaye kurejea kijijini, ambapo hupata msaada unaofaa wakati wa ujauzito wake.

Usiku mmoja ndani ya kijiji cha wanawake

Kuwasili kwangu kunaleta hisia tofauti. Kwanza kabisa, natambulishwa kwa mratibu wa jamii, ambaye anaonekana kupendwa na kuheshimiwa kutokana na mapokezi ya kirafiki anayopata kutoka kwa kila mwanamke kijijini.

“Huyu anaitwa Kevin,” analiambia kundi lake la kina mama.

“Tumemkaribisha akae hapa usiku wa leo ili aone jinsi tunavyoishi. Tafadhali msimfukuze.”

Wanawake hao wanacheka, na baada ya majadiliano wanakubali ombi lake. Hivyo ninaruhusiwa kukaa, lakini kwa usiku mmoja tu, wanasema, chini ya uangalizi wao.

Ninalala peke yangu, juu ya sehemu iliyotengenezwa kwa ngozi ya mbuzi.

Ulikuwa ni usiku uliotulia, ambapo mara kwa mara nilisikia sauti za ving’ora. Ninalala bila usumbufu.

Asubuhi na mapema, niliamshwa na milio ya ndege na nyimbo za Kisamburu kutoka kwa wanawake walionikaribisha.

Pauline alikuwa nje ya mlango ya chumba nilicholala, akinisubiri kwa hamu.

“Ulilalaje?” aliniuliza.

“Vizuri sana na kwa amani,” nami nilimjibu.

“Unaona,” anasema, “kuna amani hapa na pia tunawapenda wanaume wetu.”

Mwanamke mwingine alionekana kucheka huku akisema, “Tunawapenda sana. Hatutaki tu wawe ndani ya kijiji chetu.”

Pauline ananipa mswaki wa kijiti na kutabasamu huku nikinawa uso wangu kwa kutumia maji yaliyo katika kibuyu.

Jambo moja lilikuwa wazi kwangu: Hapa ndio ilikuwa sehemu salama kwa kina mama hawa. Na kamwe, hawawezi kuifutilia mbali amani wanayosema wanaipata hapa.

Baadae nilipata fursa ya kutembezwa nje ya kuta za kijiji cha Ltungai.

Alama za nyayo za wanyama pori kama fisi zilionekana, hii ikiwa ni uthibitisho wa hatari ambazo wanawake hawa wanatakiwa kukabiliana nazo.

“Tuko na amani hata hivyo,” mkazi mmoja anasema. “Tukiogopa, tutaenda wapi? Turudi kuteseka?”

Ni mipaka tu, Sio chuki kwa wanaume

Wanasisitiza jambo moja: kijiji hiki hakijajengwa kuonesha chuki dhidi ya wanaume.

“Kama mwanaume atakuja hapa bila ruhusa yetu,” mwanamke mmoja atamuonya, “Atajuta kwa nini alikuja.”

Wanawake hao wanasema watamfukuza kwa pamoja nje ya kijiji, wakitumia silaha ya umoja wao.

“Hatuwachukii wanaume,” mwingine anaeleza. “Lakini kwa sababu ya yale waliyotufanyia, hatuwataki hapa. Hii ni nafasi yetu sisi tu.”

Wanavyoishi

Maisha hapa si rahisi.

Kila asubuhi, baadhi ya wanawake hutembea umbali mrefu kwenda timboni, ambako huchimba na kuchuja mawe yanayotumika katika ujenzi kwa ajili ya kujipatia kipato.

Wengine hutengeneza vito na mapambo kwa kutumia shanga, na kuuza kwa wasafiri au watalii wanaopita.

“Kama jirani yako ana chakula na wewe huna,” mwanamke mmoja ananiambia, “Tunasaidiana.”

Licha ya ugumu wa maisha, wanawake wanasema wanahisi wako salama zaidi kuliko mahali popote walipowahi kuishi awali.

Kijiji cha Ltungai kinaendelea kuwa sehemu salama, inayotoa ulinzi kwa wale wote wanaoishi ndani ya kuta zake.