Wafanyabiashara Tanzania wafurahia marufuku ya raia wa kigeni kufanya kibiashara ndogo ndogo
Raia wa kigeni amabao bado wanafanya kati ya biashara 15 zilizopigwa marufuku wanaruhusiwa kuendelea hadi leseni zao zitakapokwisha.
Wafanyabiashara Tanzania wafurahia marufuku ya raia wa kigeni kufanya kibiashara ndogo ndogo
Raia wa kigeni hawaruhusiwi kufanya uchimbaji mdogo wa madini Tanzania / wizara ya madini Tanzania / Public domain
30 Julai 2025

Wafanyabiashara nchini Tanzania wameipongeza serikali kwa kuweka sheria kali za kutetea wazawa ili wanufaike zaidi kiuchumi. Wengine wamesema hatua hiyo imekuja wakati muafaka.

Serikali katika ilani yake iliyochapishwa 25 Julai 2025, imepiga marufuku aina 15 za biashara ambazo raia wa kigeni hawaruhusiwi kujihusisha nazo.

Baadhi ya mauzo ya jumla na reja reja, huduma za miamala ya simu, ukarabati wa simu za mkononi na vifaa vya kielektroniki na biashara ya saluni isipokuwa katika hoteli au kwa madhumuni ya utalii ni maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya raia wa Tanzania pekee.

“Faini isiyopungua zaidi ya dola 3800 (shilingi milioni 10 ) au kifungo kisichozidi miezi 6 na kunyimwa visa na kibali cha makazi ni adhabu itakayotolewa kwa raia wa kigeni wanaopatikana kukiuka sheria hii,” Gazeti ya Serikali la 29 Julai 2025, imesema.

Huduma ya usafishaji wa nyumba, ofisi na mazingira, uchimbaji mdogo wa madini, huduma za posta na usafirishaji wa mizigo, huduma kama waongozaji wa watalii na uendeshaji wa makampuni ya redio na televisheni pia yamepigwa marufuku kwa raia wa kigeni.

“Iwapo raia wa Tanzania atamsaidia mgeni kufanya biashara hizo faini ya dola 1,900 (shilingi milioni 5) au kifungo kisichozidi miezi mitatu jela kitampata akipatikana na hatia,” serikali imesema.

Uendeshaji wa maeneo ya makumbusho na maduka ya vito vya sanaa, madalali wa nyumba, ununuzi wa chakula kutoka mashambani, umiliki au uendeshaji wa vituo vya kamari na umiliki wa biashara ndogo ndogo umebaki kwa raia wa Tanzania pekee.

Wale ambao tayari wana leseni ya biashara hizi wanaruhusiwa kuendelea hadi leseni zao zitakapokwisha.

CHANZO:TRT Swahili