Licha ya mashambulizi ya anga ya Israel kuendelea Gaza, makubaliano mapya ya usitishaji mapigano yameanza kuonekana katika eneo hilo lililoharibiwa vibaya, huku misafara ya misaada ikivuka mpaka wa Rafah chini ya masharti ya mkataba ambao wengi waliamini usingewezekana.
Katika kiini cha mafanikio hayo yasiyotarajiwa Uturuki ina nafasi kubwa, nafasi yake kama mpatanishi na mdhamini ilibadilisha mwelekeo wa mazungumzo yaliyokuwa yakionekana kuyumba.
Wakati Rais wa Marekani Donald Trump alipotoa Mpango wa Amani wa Gaza wenye vipengele 20 mnamo Septemba 29, majibu yalikuwa ya tahadhari.
Mpango huo uliahidi kumaliza mapigano, kubadilishana wafungwa, na kuruhusu misaada ya kibinadamu bila vizuizi, lakini uliacha mapengo makubwa.
Haukutoa utaratibu wa utekelezaji, muda maalum wa kuondoka kwa wanajeshi, wala wadhamini wa kuaminika kuhakikisha pande zote zinatii masharti.
Kwa Hamas, ambayo bado ilikuwa inajikokota baada ya mauaji ya miaka miwili yaliyofanywa na Israel, pendekezo hilo halikuonekana kutoa ulinzi wala uwajibikaji wowote.
Wakosoaji walidai mpango huo ulikuwa zaidi ya maigizo ya kisiasa kuliko sera halisi, wakitaja tangazo la upande mmoja la Trump na ukosefu wa mashauriano na wapatanishi muhimu kama Misri na Qatar.
Hamas, kwa upande wake, ilisisitiza kwamba haitazingatia suala la kuachilia silaha au wafungwa bila “dhamana za kisheria” — jambo ambalo Uturuki baadaye ililikubali na kulitekeleza.
Jinsi Uturuki ilivyobadilisha mwelekeo
Uturuki iliitwa kushiriki katika mazungumzo ya Sharm El-Sheikh, ishara ya uaminifu wa Ankara kwa Hamas na uhusiano wa karibu wa kibinafsi kati ya Trump na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.
Ujumbe wa Uturuki uliongozwa na mkuu wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (MIT), Ibrahim Kalin, aliyewakilisha diplomasia ya kisiasa ya Ankara na kuratibu ushirikiano wa utendaji kazi.
Alisaidia kueleza maono ya Uturuki kuhusu usitishaji wa mapigano wa kuaminika huku akiratibu mawasiliano kati ya maafisa wa Hamas, Marekani, Misri, na Qatar.
Lakini kabla ya yote, kulitanguliwa na ziara muhimu na yenye mafanikio ya Rais Erdogan nchini Marekani, ambapo alijadiliana na Rais Trump kuhusu masuala nyeti, ikiwemo suala la Palestina.
Alhamisi, Trump alikiri hadharani mchango wa Erdogan katika kufanikisha makubaliano hayo.
Wachambuzi wa mazungumzo ya Sharm El-Sheikh walibaini kwamba ushiriki wa Uturuki ulisaidia kuleta uhalisia na mpangilio katika mazungumzo yaliyokuwa yamekwama.
Mazungumzo hayo yalijumuisha pendekezo la mfumo wa wadhamini wanne — Uturuki, Misri, Qatar, na Marekani — ili kuhakikisha utekelezaji, kufuatilia ukiukaji wa makubaliano, na kuratibu mabadilishano ya wafungwa.
Ingawa majukumu ya kila nchi bado yalikuwa yakibainishwa, mfumo huo ulionyesha juhudi za pamoja za kudumisha usitishaji mapigano.
Mfumo huo ulijibu moja kwa moja madai muhimu ya Hamas: uwepo wa wadhamini wanaoaminika watakaokomesha hatua za upande mmoja za Israel.
Pia uliipa Marekani njia ya kisiasa ya kuwahakikishia pande zinazopigana. Ushiriki wa Ankara, ambao awali ulitazamwa kwa mashaka na Tel Aviv, hatimaye ulionekana kuwa muhimu katika kupata ridhaa ya Hamas.
Matokeo yake, pendekezo la Marekani lililokuwa halifahamili lilibadilishwa kuwa mpango ulioeleweka, unaofuatiliwa, na unaotekelezeka kwa hatua. Ndani ya siku chache baada ya Uturuki kujiunga, pande zote mbili zilikubaliana juu ya muhtasari wa makubaliano yaliyopata uungwaji mkono wa wapatanishi wakuu wote.
Kwa nini usitishaji huu ni tofauti
Makubaliano haya ni tofauti na yale mawili yaliyotangulia — moja mwishoni mwa 2023 na jingine mapema 2025 — yote yakishindikana kutokana na mashambulizi ya Israel kuendelea na ukosefu wa mifumo thabiti ya utekelezaji.
Safari hii, mfumo wa wadhamini wengi — wenye majukumu yaliyobainishwa, ufuatiliaji wa wakati halisi, na kamati ya ufuatiliaji — umeunda muundo wa utekelezaji ambao haujawahi kuonekana katika makubaliano ya awali.
Chini ya masharti mapya, mabadilishano ya wafungwa na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu vimepangwa kwa hatua. Silaha zitagawanywa katika makundi mawili: za “kujilinda” na za “kushambulia,” ambapo zile za kujilinda zitahamishwa hatua kwa hatua kwa mamlaka mpya ya kiufundi ya Palestina.
Ofisi ya kisiasa ya Hamas ilikubali pendekezo hilo.
Makubaliano yalihitimishwa jana huko Sharm El-Sheikh, na ndani ya saa chache, malori ya misaada yalianza kuingia Gaza kupitia Rafah — ishara ya kwanza ya utekelezaji wa usitishaji.
Saudi Arabia na Jordan, ingawa si wapatanishi wakuu, zilishiriki katika mazungumzo hayo kutoa uhalali wa kikanda na msaada wa kisiasa kwa ajili ya kurejesha usalama na uthabiti wa Gaza.
Kwa Uturuki, usitishaji huu wa mapigano ni zaidi ya ushindi wa kidiplomasia; ni uthibitisho wa kimkakati wa kanuni zake za muda mrefu za sera ya nje: kwamba amani endelevu Mashariki ya Kati inategemea suluhisho la mataifa mawili, uongozi halali wa Kipalestina, usawa wa kibinadamu, na dhamana thabiti za usalama.
Rais Erdogan tayari ameahidi ushiriki wa Uturuki katika kikosi cha kimataifa kitakachosimamia utekelezaji wa makubaliano na kutafuta mateka wa Kiyahudi waliopotea.
“Kwa mapenzi ya Mungu,” alisema, “Uturuki itashiriki katika kikosi cha kuhakikisha makubaliano haya yanadumu.”
Usitishaji huu wa mapigano umebadilisha nafasi ya kidiplomasia ya Uturuki katika eneo hili. Uwezo wake wa kushirikiana kwa ufanisi na washirika wa Magharibi na wa Kiarabu umeimarisha sifa yake kama mpatanishi wa kuaminika — mwenye busara, anayeaminika, na anayejua kutafsiri malengo magumu ya kisiasa kuwa mipango inayotekelezeka.
Ikiwa makubaliano haya yatadumu, yatakuwa ushahidi kwamba amani ya kweli inahitaji dhamira ya kisiasa pamoja na wadhamini wa vitendo. Uturuki imetoa vyote viwili.
Kwa Gaza, hii inamaanisha fursa tete lakini hali halisi ya kupona — mradi tu mashambulizi ya Israel yakome na pande zote ziheshimu usitishaji.
Kwa Uturuki, ni uthibitisho wa sera yake ya nje inayochanganya maadili na uwezo wa kimkakati, huku ikiweka tena suluhisho la mataifa mawili katikati ya juhudi za amani Mashariki ya Kati.