Disemba inapoingia, kama ilivyo kawaida, wengi walianza kujiandaa kwa ajili ya mapumziko ya mwisho wa mwaka. Pengine kusafiri vijijini kwa ajili ya kutembelea ndugu, jamaa na marafiki ili kupumzisha akili baada ya pirika za mwaka mzima.
Lakini wiki moja tu ndani ya mwezi wa Disemba, habari za kushtukiza kutoka Afrika Magharibi zikaenea mitandaoni.
Ni kuhusu wanajeshi wa Benin ambao walifanya jaribio la kuchukua nchi na kutangaza kumuondoa madarakani Rais wa nchi hiyo Patrice Talon.
Kupitia televisheni ya taifa, wanajeshi hao wakiongozwa na Luteni Kanali Pascal Tigri walitangaza kupinduliwa kwa Patrice Talon, rais wa Benin, wakidai kufanya shambulio dhidi ya makazi yake huko Cotonou na makazi ya maafisa wengine wa ngazi za juu wa jeshi.
Hata hivyo, hayo yalikuwa mapinduzi mafupi zaidi kushuhudiwa Afrika kwani saa chache tu baadaye, serikali ilitangaza kuyazima na kuwakamata baadhi ya waliopanga njama hiyo.
Hali ya hivi punde Benin
Udhibiti wa serikali umerejeshwa nchini kote, ingawa takriban wanajeshi 200 wa Afrika Magharibi (hasa Nigeria na Ivory Coast) wamesalia kusaidia kulinda nchi.
Mamlaka imeanzisha uchunguzi na kutoa vibali vya kimataifa vya kukamatwa kwa wanaodaiwa kuunga mkono mapinduzi hayo.
Lakini japo Rais Talon wa Benin alifanikiwa kushikilia uongozi wake, wengine waliondolewa na hata kulazimika kukimbia nchi kwa usalama wao.
Uchaguzi ujao wa rais wa Benin bado umepangwa kufanyika Aprili 2026, na Rais Talon, anatarajiwa kukamilisha muhula wake.
Guinea-Bissau- Mapinduzi kamili (Novemba 26, 2025)
Tarehe 26 Novemba 2025, maafisa wa kijeshi wa Guinea Bissau walimkamata Rais Umaro Sissoco Embaló na kutangaza kuwa wamechukua udhibiti wa serikali. Mapinduzi hayo yalifanyika muda mfupi kabla ya matokeo ya mwisho ya uchaguzi mkuu wa Novemba 23 kutangazwa, hatua iliyozidisha mvutano wa kisiasa.
Guinea-Bissau imekumbwa na mizozo ya kisiasa ya mara kwa mara kwa miaka mingi, ikichangiwa na vita vya kutaka madaraka na changamoto kubwa za kiusalama.
Hali ya hivi punde
Maandamano yamefanyika mjini Bissau kulaani mapinduzi hayo na kutaka viongozi wa upinzani waliozuiliwa waachiliwe.
Utawala wa kijeshi - ambao sasa unaongozwa na Meja-Jenerali Horta Inta-A Na Man - umezindua katiba ya mpito ya miezi 12 ambayo inazuia kiongozi wa sasa wa muda na Waziri Mkuu kugombea katika uchaguzi.
ECOWAS imepangwa kujadili uwezekano wa vikwazo na majibu katika mkutano huko Abuja, Nigeria.
Bado hakuna tarehe thabiti ya uchaguzi iliyotangazwa; katiba ya mpito inapendekeza angalau mwaka wa utawala unaoongozwa na jeshi kabla ya kurudi tena kwa uchaguzi wa kiraia, lakini ratiba hii inapingwa na mashirika ya kiraia na makundi ya kisiasa.
Madagascar-Mapinduzi kamili (Oktoba 2025)
Mnamo Oktoba 2025, huku kukiwa na maandamano makubwa yaliyoongozwa na vijana dhidi ya ufisadi, ukosefu wa ajira na huduma duni, kitengo cha jeshi kinachojulikana kama CAPSAT kilijitenga na kutangaza kuchukua udhibiti wa nchi.
Rais wa wakati huo, Andry Rajoelina, alikimbia nchi na kushtakiwa na wabunge. Viongozi wa kijeshi walitangaza mapinduzi na kumtaja Kanali Michael Randrianirina kuwa kiongozi mpya.
Madagascar imekuwa na vipindi vya machafuko ya kisiasa na uchaguzi uliopingwa hapo awali, lakini udhibiti kamili wa kijeshi haukuwa kitu cha kawaida. Unyakuzi wa 2025 unafuatia miezi ya kuongezeka kwa mfadhaiko wa umma na kuvunjika kwa imani na serikali yao.
Hali ya hivi punde Madagascar
Mtawala mpya wa kijeshi amesimamisha taasisi kuu za kisiasa, zikiwemo katiba na vyombo vya uchaguzi.
Awali serikali ilikadiria uchaguzi ndani ya miezi 18 hadi miaka miwili, lakini hili bado limegubikwa na utata.
Harakati sambamba za kurejesha utawala wa kiraia zinaongezeka miongoni mwa makundi ya upinzani.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, uchaguzi unatarajiwa mapema zaidi ya katikati ya 2027 ikiwa jeshi litaweka ratiba yake iliyotangazwa. Hata hivyo, hakuna ramani inayotambulika kimataifa ya kurudi katika utawala wa kiraia.
Mali - Jaribio la mapinduzi lililotibuka (Agosti 2025)
Mamlaka nchini Mali iliwakamata maafisa wa kijeshi na raia wanaotuhumiwa kupanga njama dhidi ya utawala wa kijeshi wa Mali. Haya yanajiri huku nchi hiyo ikisalia chini ya udhibiti wa kijeshi kufuatia mapinduzi ya mwaka 2020 na 2021.
Uchaguzi wa urais ulipangwa kufanyika nchini Mali tarehe 27 Februari 2022, kufuatia mapinduzi ya 2021. Baada ya kuahirishwa, mnamo Julai 2022 uchaguzi uliratibiwa upya hadi tarehe 4 Februari 2024. Mnamo Septemba 2023, uongozi wa kijeshi ulisema kwamba uchaguzi "utaahirishwa kidogo kwa sababu za kiufundi," bila kutoa tarehe mpya.
Burkina Faso - Jaribio la mapinduzi lililotibuka (Aprili 2025)
Serikali ya kijeshi inayotawala iliripoti kwamba ilizuia mapinduzi yaliyopangwa, ambayo yanadaiwa kuhusisha askari wa sasa na wa zamani wenye uhusiano wa nje.
Uchaguzi uliokusudiwa kurejesha serikali ya kiraia ya kidemokrasia nchini Burkina Faso mnamo Julai 2024 haukupewa "kipaumbele" na uliahirishwa kwa muda usiojulikana na utawala wa kijeshi unaoongozwa na Kapteni Ibrahim Traoré tangu alipochukua madaraka kwa nguvu Septemba 2023.
Katika maeneo ya Afrika Magharibi na Kati, mapinduzi ya hivi karibuni na majaribio ya mapinduzi yameibua wasiwasi kuhusu utaratibu wa kikatiba. ECOWAS imetangaza hali ya hatari ya kikanda ili kukabiliana na "wimbi hili la mapinduzi" na kuahidi hatua iliyoratibiwa ili kuhifadhi utawala wa kikatiba.
Msururu huu wa mapinduzi na majaribio ya mapinduzi wakati mwingine hujulikana kama "Ukanda wa Mapinduzi ya Afrika," kuonyesha jinsi mapinduzi ya kijeshi yalivyojikita katika eneo hilo huku kukiwa na taasisi dhaifu, matatizo ya kiuchumi, na mgawanyiko wa kisiasa.
Muungano wa Afrika AU umeendelea kukemea hatua zozote za mapinduzi ya kijeshi. Mashirika na taasisi za kikanda na bara zima limetumia diplomasia na upatanishi ili kuzuia kuzorota kwa hali ya usalama.













