Afrika Kusini imeruhusu kuingia kwa wakimbizi zaidi ya 150 kutoka Gaza, Palestina. Wapalestina hao wamewasili kutoka Kenya kwa ndege maalum kutafuta hifadhi, baada ya hapo awali kuzuiwa kuingia kutokana na kutokidhi masharti ya uhamiaji.
Mamlaka ya Usimamizi wa Mipaka ilisema wakimbizi hao hawakutoa maelezo kuhusu muda wao wa kukaa nchini humo au makazi waliyokusudia, na pia hawakuwa na mihuri ya kuondoka kwenye pasipoti zao.
"Abiria pia hawakuwa na mihuri ya kuondoka katika pasipoti zao," Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mipaka, Michael Masiapato alisema.
Wapalestina hao walilazimika kusubiri zaidi ya saa 10 katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa OR Tambo, suala lililoibua hasira miongoni mwa wanaharakati nchini humo, wanaojulikana kwa msimamo wao thabiti wa kuunga mkono haki za Wapalestina.
Afrika Kusini iliwasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko The Hague mnamo Desemba 29, 2023, ikiishutumu Israel, ambayo imeshambulia Gaza tangu Oktoba 2023, kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake chini ya Mkataba wa Mauaji ya Halaiki ya 1948.
Kuingia Afrika Kusini kwa masharti
Serikali ya Afrika Kusini pia imesema mara kadhaa kwamba inasimama pamoja na watu wa Palestina.
Mamlaka ya Usimamizi wa Mipaka, hata hivyo, ilisema ilipokea barua kutoka kwa shirika la misaada ya kibinadamu la Gift of the Givers Foundation ikisema kwamba itawapa makazi wasafiri wakati wa kukaa kwao nchini humo.
Masiapato alisema Wapalestina wanastahili kupata msamaha wa viza ya siku 90 kusafiri hadi Afrika Kusini na wameshughulikiwa kama kawaida na watatakiwa kuzingatia masharti yote ya kuingia nchini humo.
"Kufikia wakati wa kuingia nchini, 23 kati ya 153 (Wapalestina) walikuwa tayari wamehamishwa kutoka Afrika Kusini hadi nchi wanazoelekea," Mamlaka ya Usimamizi ilisema, na kuongeza kuwa wengine 130 walibaki nchini chini ya uangalizi wa Wakfu wa Gift of the Givers.
Imtiaz Sooliman, mwanzilishi na mwenyekiti wa Wakfu wa Gift of the Givers, alisema katika taarifa yake kwamba Israel haikuwapigia Wapalestina mihuri ya kutoka katika pasipoti zao walipoondoka.
Kupata nafuu
"Israel kwa makusudi haikugonga muhuri pasipoti za watu hawa maskini (ili) kuzidisha mateso yao katika nchi ya kigeni," alisema.
Wapalestina walionyesha kufurahi baada ya kuruhusiwa kuteremka kutoka kwa ndege yao. Walikaribishwa na wanafamilia, marafiki na vikundi vinavyounga mkono Palestina.
"Ninashukuru kuwa hapa. Nilidhani hawataturuhusu kuingia. Sasa ninaweza kwenda Cairo na kujiunga na familia yangu huko," mwanafunzi mdogo wa kike wa Kipalestina aliwaambia waandishi wa habari.
Alisema anatarajia kuendeleza masomo yake nchini Misri.
Sooliman alimshukuru Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Ronald Lamola na Zane Dangor, mkurugenzi mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini (DIRCO), kwa kuja kuwaokoa wakimbizi wa Kipalestina waliokwama.
Alisema Lamola alichukua hatua ya kuiandikia barua Idara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambayo iliondoa hitaji la muhuri wa kuondoka ili kuwaruhusu Wapalestina kuingia.
Ilikuwa ni ndege ya pili kuwasafirisha Wapalestina waliokuwa wakikimbia mauaji ya halaiki huko Gaza hadi Afrika Kusini.
Ndege ya kwanza ilitua mwishoni mwa mwezi uliopita katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo ikiwa na Wapalestina 176.





















