AFRIKA
2 dk kusoma
Mgombea wa upinzani Cameroon Tchiroma atoa wito wa maandamano kabla ya matokeo
Maafisa wamepiga marufuku mikusanyiko ya umma na safari za boda boda katika miji mbalimbali wakati wakisubiri kutangazwa kwa matokeo ya mwisho kufikia Jumatatu jioni.
Mgombea wa upinzani Cameroon Tchiroma atoa wito wa maandamano kabla ya matokeo
Tchiroma Bakary amedai kushinda uchaguzi wa urais. / Reuters
tokea masaa 6

Waziri wa zamani wa serikali na mgombea urais Issa Tchiroma Bakary ametoa wito kwa raia wa Cameroon kujitokeza kwa maandamano iwapo Mahakama ya Katiba itatangaza "matokeo ya uwongo na yaliyochakachuliwa" katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa.

Rais wa sasa Paul Biya, 92, anatafuta kuingia madarakani kwa muhula wa nane utakaomfanya awepo uongozini kwa zaidi ya miaka 43.

Wanaomuunga mkono Tchiroma, ambao kulingana na hesabu za matokeo yake mwenyewe ni asilimia 54.8 ya kura dhidi ya asilimia 31.3 za Biya, wamekuwa wakijitokeza kuandamana mara moja moja tangu wiki iliyopita na kudai ushindi kwenye uchaguzi wa urais.

Kufikia Jumatano, maafisa walikuwa wamepiga marufuku mikusanyiko ya watu hadharani na safari za boda boda katika miji kadhaa wakati wakisubiri matokeo rasmi yanayotarajiwa kufikia Jumatatu jioni.

"Matangazo hayo ya matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais wa Oktoba 12, 2025, yatafanyika siku ya Jumatatu, Oktoba 27, saa tano asubuhi," kulingana na taarifa iliyotolewa na Baraza la urais Jumatano jioni.

"Tujitokeze kwa ajili ya ukombozi na kudai ushindi wetu," Tchiroma alisema kupitia njia ya video katika mtandao wa Facebook, akiwataka wanaomuunga mkono kuwa "kitu kimoja katika suala la amani na kwa mapenzi ya nchi yetu."

Chama cha RDPC cha Biya kimepinga madai ya ushindi wa Tchiroma na kutaja hatua hiyo kama "ulaghai" na "uwizi usiokubalika katika nchi inayofuata sheria", wakisema katika taarifa kuwa "wanasubiri kwa hamu matokeo rasmi".

CHANZO:TRT Afrika Swahili