Serikali ya Rwanda imetangaza mipango ya kuwekeza hadi dola bilioni 1 (zaidi ya Rwf1,440 bilioni) katika uzalishaji wa nishati ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na uanzishaji wa viwanda.
Akizungumza muda mfupi baada ya kutangazwa kwa tozo mpya za umeme, Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi, Yusuf Murangwa, alisema miradi muhimu ni pamoja na vyanzo vya nishati mbalimbali, vikiwamo vya umeme wa jua na teknolojia ya nuklia.
"Kwa sasa tunazalisha takriban megawati 400 (MW). Lakini hivi karibuni, tuseme katika miaka mitano, tutahitaji takriban MW 1,000 ili kuweza kukidhi mahitaji ya nishati ya viwanda na huduma za teknolojia, kama vile vituo vya takwimu,” Murangwa alisema.
“Hii itahitaji uwekezaji wa dola bilioni moja katika kipindi hicho," Murangwa alisema katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Taifa RBA.
Waziri huyo alisema idadi ya kaya za Rwanda zilizounganishwa na umeme imeongezeka kutoka asilimia 2 mwaka 2000 hadi 75 mwaka 2025.
Serikali inalenga kufikia asilimia 100 ya upatikanaji wa umeme ifikapo 2029.
"Katika kipindi cha miaka 25, serikali ilifanya uwekezaji mkubwa katika uzalishaji na usambazaji wa nishati, lakini hiyo haitoshi," alisema Murangwa.
"Katika kipindi cha miaka minne hadi mitano ijayo, tutahitaji kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa nishati ili kufikia upatikanaji wa kaya na kukidhi mahitaji ya nishati kwa viwanda na huduma."
Kwa sasa kuna miradi inayoendelea kama ya megawati 250 ya Nyabarongo Hydroelectric Project II, mradi ujao wa umeme wa jua wa megawati 200.
Alisema serikali ina malengo yake katika kuzalisha nishati ya nyuklia na kuwa mradi huo wa nyuklia bado unafanyiwa utafiti na huenda ukakamilika katika kipindi cha miaka mitatu hadi mitano ijayo.
Miradi mingine ambayo inaelekea kuongeza uwezo wa kuzalisha nishati nchini Rwanda ni pamoja na uchimbaji wa gesi ya methane kutoka Ziwa Kivu, ambayo inaweza kuzalisha hadi Megawati 156.