Rais wa Kenya William Ruto alisema Jumatano kuwa nchi yake inatarajia kusaini makubaliano ya kibiashara na Marekani kabla ya mwisho wa mwaka huu, na kwamba atashinikiza Washington kuongeza mkataba wa biashara usio na ushuru na Afrika kwa angalau miaka mitano.
Ruto alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio Jumatano kujadili Sheria ya Fursa za Ukuaji wa Afrika (AGOA).
Sheria hiyo ya miaka 25 inatoa mataifa ya Afrika yanayostahili fursa ya kuingiza bidhaa zao kwenye soko la Marekani bila ushuru, lakini inatarajiwa kumalizika muda wake mwezi huu.
"Nitamuomba atilie uzito suala la kuhuisha na kuongeza muda wa AGOA kwa angalau miaka mitano, kwa sababu ni jukwaa linalounganisha Afrika na Marekani kwa njia ya msingi sana, na linaweza kusaidia sana kutatua baadhi ya changamoto za biashara zilizopo sasa," alisema Ruto kabla ya mkutano huo.
Ruto alisema anaamini kuwa utawala wa Marekani umeongeza kuthamini kwake AGOA.
Kupanua na kuimarisha mahusiano
Juhudi za pande mbili za kuhakikisha AGOA inaongezwa mwaka jana hazikufanikiwa kupata kura katika Bunge la Marekani. Kurudi kwa Rais Donald Trump Ikulu ya Marekani mwezi Januari, akiwa na sera yake ya biashara inayotegemea ushuru, kumeongeza mashaka kuhusu kuongezwa kwa mkataba huo.
"AGOA inatoa nafasi bora kwa Afrika na Marekani kupanua na kuimarisha biashara," alisema Ruto.
Ruto alisema kuwa Marekani na Kenya zimepiga hatua nzuri kuelekea makubaliano ya kibiashara ya pande mbili, na akaongeza kuwa anatarajia kusaini makubaliano hayo kabla ya mwisho wa mwaka 2025. Mnamo Aprili, Trump aliweka ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa za Kenya.
Kenya inatafuta fursa ya kuingiza bidhaa zake kama mavazi, nguo, na mazao ya kilimo kama chai, kahawa, na parachichi kwenye soko la Marekani.
Ya Kwanza ya Aina Yake
Ruto anataka kuchunguza maeneo mapya kama uchimbaji madini na uvuvi. Ikiwa makubaliano yatafikiwa, yatakuwa ya kwanza ya aina yake kati ya taifa la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Washington.
Ruto alisema Kenya ina makubaliano thabiti ya kibiashara na washirika kadhaa, ikiwemo China ambayo imeondoa ushuru wote kwa bidhaa za kilimo kutoka nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
"Tuna nakisi ya biashara kwa faida ya China, lakini ile ya Marekani ni ya uwiano mzuri, hivyo bado tunatafuta njia za kusawazisha biashara na washirika wetu wote wa kibiashara," alisema.
Mapema Jumatano, Ruto aliliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa wakati Kenya imejitokeza nchini Haiti kuongoza kikosi cha kimataifa kupambana na magenge yenye silaha, dunia haijajitokeza kusaidia taifa hilo la Karibiani na ujumbe huo unakosa msaada wa vifaa.
"Tunahitaji idadi kubwa zaidi," Ruto aliiambia Reuters. "Tunahitaji vifaa zaidi, tunahitaji msaada wa kifedha zaidi ili kuweza kufanikisha hili."
Magenge yenye silaha yamechukua udhibiti wa karibu mji mkuu wote wa Haiti, Port-au-Prince, katika mzozo ambao umewalazimisha takriban watu milioni 1.3 kuhama makazi yao, na kuchochea njaa.