AFRIKA
2 dk kusoma
DRC na Rwanda wamekubaliana kuanza kutekeleza hatua za kiusalama mwezi wa Oktoba
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda wamekubaliana kuanza kutekeleza hatua za kiusalama chini ya makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani mwezi ujao, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumatano.
DRC na Rwanda wamekubaliana kuanza kutekeleza hatua za kiusalama mwezi wa Oktoba
Baadhi ya wakimbizi wa ndani hawakuweza kurudi nyumbani kwa sababu nyumba zao ziliharibiwa wakati wa mapigano. / / Reuters
tokea masaa 13

Hii ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa mkataba wa amani huku kukiwa na wasiwasi kuhusu kucheleweshwa kwa mafanikio.

Makubaliano hayo, yaliyofikiwa katika mkutano uliofanyika Washington Septemba 17-18 na kuripotiwa kwa mara ya kwanza na shirika la habari la Reuters, yataanza kutekelezwa Oktoba 1, kwa mujibu wa taarifa hiyo ya pamoja ambayo pia imetolewa na Marekani, Qatar, Togo na Tume ya Umoja wa Afrika.

Nchi hizo zimekubaliana kukamilisha utekelezaji wa hatua hizo kufikia mwisho wa mwaka huu, kwa mujibu wa vyanzo vitatu vilivyozungumza na Reuters. Operesheni za kuondoa tishio kutoka kwa kikundi cha waasi cha Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) kilichopo DRC, pamoja na kuwezesha kuondoka kwa majeshi ya Rwanda, zitaanza kati ya Oktoba 21 na 31, kulingana na vyanzo hivyo.

Ratiba hiyo imetoa tarehe maalum kwa Rwanda na DRC kutekeleza mpango wa amani huku kukiwa na wasiwasi kwamba mpango huo unakumbwa na changamoto.

Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC na Rwanda walitia saini mkataba wa amani mjini Washington mnamo Juni 27, na kukutana siku hiyo hiyo na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye ana nia ya kuvutia uwekezaji wa mabilioni ya dola kutoka nchi za Magharibi katika eneo hilo lenye utajiri wa madini kama tantalum, dhahabu, kobalti, shaba, lithiamu na madini mengine.

Mkataba huo pia ulikuwa na ahadi ya kutekeleza makubaliano ya mwaka 2024 ambayo yalieleza kuwa Rwanda ingeondoa hatua zake za kiulinzi ndani ya kipindi cha siku 90.

Operesheni za kijeshi za DRC dhidi ya FDLR — kikundi cha waasi kilichopo Congo ambacho kinajumuisha wanajeshi wa zamani wa Rwanda na wanamgambo waliohusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 — zinapangwa kukamilika ndani ya muda huo huo wa siku 90.

Muda huo wa siku 90 wa makubaliano ya awali ya 2024 unakamilika Alhamisi. Chanzo kimoja kilisema muda haukuanza kuhesabiwa kuanzia siku mkataba uliposainiwa, bali ulipangwa kuanza baada ya mkutano wa kwanza wa kikosi kazi kipya cha ushirikiano wa kiusalama uliofanyika Agosti 7-8.

Katika mkutano wa Septemba uliofanyika Washington, DRC na Rwanda walijadiliana agizo la utekelezaji (operational order) la kuendeleza makubaliano hayo ya 2024 na kukubaliana kuanza utekelezaji mnamo Oktoba 1, kulingana na taarifa ya pamoja.

Wanachama wa kikosi kazi hicho pia walibadilishana taarifa za kijasusi ili kupata uelewa wa hali halisi mashinani, na taarifa hizo zilitumika kuandaa mpango wa hatua kwa hatua wa kuondoa kikundi cha FDLR, pamoja na kuondoa majeshi na hatua za kiulinzi zilizowekwa na Rwanda, kwa mujibu wa taarifa hiyo.

CHANZO:Reuters