Kiongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ameomba nchi wanachama za Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne kutambua "mauaji ya kimya kimya ya halaiki" nchini kwake.
"Dalili zote za maangamizi zinaonekana sasa hivi... haya si mapigano tu, ni mauaji ya kimya kimya ya halaiki yaliyoathiri watu kwa zaidi ya miaka 30," Rais wa DRC Felix Tshisekedi alisema katika hotuba yake kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Alitoa wito wa kuwepo kwa tume huru ya uchunguzi ya kimataifa kusaidia "kuvunja mzunguko wa kutochukua hatua ambao umesababisha majanga kwa miongo kadhaa", pamoja na vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya waliohusika na "uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu, na mauaji ya halaiki" yaliyofanywa mashariki mwa nchi.
Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti ya uwezekano wa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu "uliofanywa na pande zote mbili" katika mapigano hayo.
Mapigano ya miongo mitatu
Mashariki mwa DRC ni eneo lenye utajiri mkubwa wa madini, na limekumbwa na mapigano kwa miongo mitatu.
Vurugu zimezidi tangu 2021 kutokana na uasi wa kundi la M23 dhidi ya serikali, ambalo Umoja wa Mataifa inasema linaungwa mkono na Rwanda na jeshi lake.
M23 ilidhibiti miji mikubwa ya eneo la Goma mwezi Januari na Bukavu mwezi Februari. Kulingana na Umoja wa Mataifa, mapigano ya tangu Januari yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwaondoa maelfu wengine katika makazi yao.
Waangalizi wanahofia kuhusu mashambulizi ya M23 huko Uvira, mji wa watu 500,000 katika mkoa wa Kivu Kusini ambao bado uko chini ya udhibiti wa jeshi la Congo na wanamgambo wanaounga mkono serikali.