Wakati viongozi wa dunia wakijumuika kwa ajili ya Mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa (UNGA), Marekani imependekeza mageuzi makubwa kwa ujumbe huo, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ufadhili na msaada wa moja kwa moja kutoka kwa Umoja wa Mataifa.
Alipokuwa akizungumza na Reuters mnamo Jumatano, Septemba 24, Balozi Mdogo wa Marekani nchini Haiti Henry Wooster alielezea hilo wakati ambapo ufadhili wa Marekani kwa ajili ya ujumbe huo unatazamiwa kumalizika Disemba 2025.
"Utoaji wa msaada wa Marekani kwa Misheni hiyo muda wake utaisha mwishoni mwa Disemba," Wooster alisema, alipoulizwa ikiwa Washington itaendelea kusaidia misheni hiyo ikiwa mpango huo utakataliwa.
Kikosi cha MSS kinachoongozwa na Kenya kilitumwa Haiti mwezi Juni mwaka jana lakini kimeshindwa kupiga hatua katika kukomesha magenge yenye silaha ndani na nje ya mji mkuu wa Port-au-Prince.
Misheni hiyo iliojengwa kwa kujitolea kutoka kwa nchi wanachama, imekabiliwa na uhaba wa fedha, askari na vifaa kama vile magari ya kivita. Takriban wanajeshi 1,000 wamepelekwa huko, kinyume na idadi iliotarajiwa ya 2,500.
Mpango mpya uliopendekezwa na Marekani, ambao utabadilisha jina la MSS kama Kikosi cha Kukandamiza Magenge na kuunda upya uongozi wake, unalenga kupeleka takriban wanajeshi 5,500, ingawa hii pia imepangwa kutolewa kwa michango ya kujitolea.
"Tunahitaji nambari zaidi," Rais wa Kenya William Ruto aliiambia Reuters katika mahojiano Jumatano.
"Tunahitaji vifaa zaidi, na tunahitaji usaidizi zaidi wa kifedha ili kuweza kutekeleza hili." Ruto aliliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York kwamba Kenya imepiga hatua kwa imani kwamba ujumbe huo ungeungwa mkono na juhudi za kimataifa.