AFRIKA
2 dk kusoma
Uganda: Museveni ateuliwa rasmi kugombea urais
Museveni aliyeingia madarakani mwaka 1986 baada ya kuuondoa utawala wa kijeshi wa Jenerali Tito Okello, ameiongoza nchi hiyo tangu kipindi hicho.
Uganda: Museveni ateuliwa rasmi kugombea urais
Rais Yoweri Museveni ameongoza Uganda tangu 1986/ picha: Reuters
23 Septemba 2025

Tume ya Uchaguzi ya Uganda siku ya Jumanne ilimuidhinisha Rais wa sasa wa Uganda Yoweri Museveni kuwania tena kiti hicho katika uchaguzi utakaofanyika mapema mwaka 2026, ambao unaweza kurefusha utawala wake katika taifa hilo la Afrika Mashariki kwa karibu nusu karne.

Museveni ameteuliwa na chama chake cha National Resistance Movement (NRM) kupeperusha bendera ya chama katika uchaguzi mkuu wa 2026 nchini humo.

Alisindikizwa na baadhi ya wanachama wa chama chake kufanya hivyo katika ofisi ya tume ya Uchaguzi.

Museveni alisema muhula mwingine wa miaka mitano madarakani utamruhusu kutekeleza kipaumbele chake cha kurejesha usalama wa umma, miundombinu ya usafiri, na kupanua huduma za afya na elimu bila malipo.

"Kuna uhalifu kidogo na kutokujali," alisema, akimaanisha wasiwasi wa umma kuhusu wimbi la uhalifu katika maeneo ya mijini.

Chama chake tawala cha National Resistance Movement pia kitafanya kazi ya "kuondoa ufisadi," alisema.

Museveni aliiingia madarakani mwaka 1986 baada ya kuuondoa utawala wa kijeshi wa Jenerali Tito Okello.

Mnamo 1996 alichaguliwa kuwa rais wa Uganda katika uchaguzi wa kwanza wa moja kwa moja wa rais nchini Uganda tangu uhuru kutoka kwa Uingereza mnamo 1962.


Tangu wakati huo ameshinda kila mchakato wa uchaguzi, na kwa sasa atakuwa anawania muhula wa saba madarakani.

Baada ya uteuzi rasmi leo chama hicho kinatarajiwa kuzindua ramani yake ya kampeni kwa Museveni na maelezo ya wapi na lini atafanya mikutano.

Chama tawala nchini NRM kinatawala bunge na serikali za mitaa kote nchini humo.


Katiba ya Uganda, iliyotungwa mwaka 1995, awali ilipiga marufuku mtu yeyote aliye na umri wa chini ya miaka 35 au zaidi ya miaka 75 kuhudumu kama rais.

Lakini mwaka wa 2005 bunge la nchi hiyo, lilifanyia marekebisho katiba ili kuondoa ukomo wa mihula ya rais na mwaka wa 2018 ilifutilia mbali ukomo huo.

Mnamo 2016 alimteua mkewe Janet Kataha Museveni kama Waziri wa Elimu na Michezo na amehudumu tangu wakati huo.

Machi 2024, Museveni alimteua mwanaye, Muhoozi Kainerugaba, Mkuu wa jeshi la Uganda.


Mwanasiasa huyo mkongwe, anasaka nafasi ya juu ya uongozi wa nchi hiyo kupitia kauli mbiu yake ya "Kulinda mafanikio".

Museveni anajinasibu kwa kuleta utulivu na maendeleo nchini Uganda na anaahidi kuwa kama atachaguliwa tena atasogeza mbele mipango ya kuifanya Uganda kuwa taifa la cha juu.

CHANZO:TRT Swahili