Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itaendelea kusimama na mfumo wa viwango kwa madini ya kobalti yanayosafirishwa nje ya nchi, na kubadilisha pale tu serikali itakapoona kuna ulazima wa kufanya hivyo, waziri wa madini wa nchi alisema siku ya Jumatano.
Waziri wa madini, Louis Watum Kabamba, ameliambia shirika la habari la Reuters katika mahojiano jijini New York kuwa nchi yake inalenga zaidi uwekezaji ambao makampuni yatachakata kobalti ndani ya nchi.
"Hatuwezi kuacha watu wengine wafanye maamuzi kwa niaba yetu. Kama kutakuwa na kobalti nyingi zaidi au la, hatufikirii hilo kwa sasa. Muhimu kwa sasa ni kupata bei nzuri," Watum alisema.
DRC, ambayo ilisafirisha asilimia 70 ya kobalti kote duniani 2024, itaanzisha mfumo wa viwango mahsusi badala ya marufuku ya kupeleka madini hayo nje ya nchi kuanzia Oktoba 16 ili kudhibiti usambazaji na bei. Wachimba madini wataruhusiwa kupeleka hadi tani 18,125 ya kobalti mwaka 2025, na kuweka kiwango cha juu kuwa tani 96,600 mwaka 2026 na 2027.
'Hatutadhibitiwa'
"Hatutadhibitiwa na China au mtu mwingine yoyote, isipokuwa sisi wenyewe. Nchi ambayo inasafirisha asilimia 70 ya kobalti kote duniani lazima iwe na sauti kuhusu bei," Watum amesema.
Kuangalia upya mifumo ya usafirishaji tutatathmini baadaye, lakini hatuwezi kusema ni muda gani, alisema.
Watum pia alisema serikali itaendelea kuchukuwa usimamizi wa baadhi ya uwekezaji iwapi watashindwa kuimarisha makampuni hayo.