AFRIKA
2 dk kusoma
Tume ya Uchaguzi Malawi yamtangaza Peter Mutharika mshindi wa uchaguzi wa Septemba 16
Aliyekuwa Rais wa Malawi Peter Mutharika amepata kura milioni 3 (aslimia 56.8) kutangazwa rasmi rais-mteule, kwa kumshinda Rais aliye madarakani Lazarus Chakwera, aliyepata kura milioni 1.77 (asilimia 33) katika uchaguzi wa Septemba 16, 2025 .
Tume ya Uchaguzi Malawi yamtangaza Peter Mutharika mshindi wa uchaguzi wa Septemba 16
Peter Mutharika, 85, alikuwa rais wa tano wa Malawi kuanzia 2014 hadi 2020. / Picha: Reuters
24 Septemba 2025

Aliyekuwa Rais wa Malawi Peter Mutharika wa chama cha Democratic Progressive Party (DPP) amethibitishwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa Septemba 16, 2025, tume ya uchaguzi ilitangaza siku ya Jumatano.

Mutharika, ambaye alikuwa rais wa tano wa Malawi kuanzia 2014 hadi 2020, alipata kura milioni 3 (asilimia 56.8) na kumshinda Rais wa sasa Lazarus Chakwera, aliyepata kura milioni 1.77 (asilimia 33).

Kulikuwa na wagombea 17 wa urais, akiwemo Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Malawi Dalitso Kabambe, aliyekuwa wa tatu na kura 211,413 (asilimia 4). Rais wa zamani Joyce Banda alipata kura 86,000 (asilimia 1.6).

Watu wasiopungua milioni 7.2 walikuwa wamesajiliwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Malawi 2025, lakini walioshiriki kwenye uchaguzi ni milioni 5.5 (asilimia 76).

Rais Chakwera akubali kushindwa

Mgombea wa urais alihitaji zaidi ya asilimia 50 za kura zilizopigwa kushinda uchaguzi katika hatua ya kwanza, na iwapo haingekuwa hivyo basi wangelazimika kushindana katika hatua ya pili kwa wagombea wawili wa nafasi ya kwanza na ya pili.

Siku ya Jumatano jioni, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi Annabel Mtalimanja alimtangaza Mutharika, 85, kuwa amechaguliwa rais baada ya kupata kura za kutosha kama ilivyotakiwa.

Mapema siku ya Jumatano, Rais anayeondoka madarakani Chakwera, 70, alikiri kushindwa na Mutharika, akisema tayari ameshampongeza rais-mteule.

Kuapishwa

Chakwera, ambaye alimshinda Mutharika katika uchaguzi wa urais wa Juni 2020, aligombea kupitia chama cha Malawi Congress Party (MCP).

Kufuatia tangazo la Jumatano la Tume ya Uchaguzi, Rais-mteule Mutharika ataapishwa ndani ya siku saba kuanzia Septemba 24, na siyo zaidi ya siku 30 kuanzia tarehe hiyo, wakati matokeo yalipotangazwa rasmi.

Mutharika, profesa wa sheria, alimchagua Mwanasheria Mkuu wa zamani na aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi, Jane Ansah, 69, kuwa mgombea wake mwenza.

CHANZO:TRT Afrika Swahili