AFRIKA
2 dk kusoma
Maelfu waandamana Malawi baada ya upinzani kuongoza katika uchaguzi wa Urais
Barabara kadhaa katika mji mkuu wa Lilongwe, zimefungwa na wafuasi wanaompinga mkuu wa Tume ya Uchauguzi ya Malawi.
Maelfu waandamana Malawi baada ya upinzani kuongoza katika uchaguzi wa Urais
Matokeo ya awali ya uchaguzi mpaka sasa yanaonesha kuwa Peter Mutharika anaongoza. / / Reuters
23 Septemba 2025

Maelfu ya wafuasi wa rais aliye madarakani wa Malawi Lazarus Chakwera ameingia mitaani katika mji mkuu wa Lilongwe, wakipinga matokeo ya awali ya uchaguzi, ambayo mpaka sasa yanaonesha kuwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Arthur Peter Mutharika anaongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu ulioisha Jumanne wiki iliyopita.

Waandamanaji walifunga barabara kadhaa katika mji huo huku wakiapa kuendelea kuandamana hadi pale “haki itakapopatikana.”

Tume ya Uchaguzi inatarajiwa kutangaza matokeo kabla ya Jumatano kama inavyotakiwa na katiba ya nchi, huku kukiwa na shinikizo la kutangaza matokeo.

“Hali ya ukiukaji”

Hivi karibuni, baadhi ya maafisa waandamizi wa chama wamekuwa wakiwataka wafuasi wao kukataa matokeo, kwa madai kwamba uchaguzi haukuwa wa haki.

Jessie Kabwila, ambae ni katibu wa MCP, ameviambia vyombo vya habari hivi karibuni kuwa chama chake hakiko tayari kukubali matokeo ya uchaguzi kwa sababu ya “ukiukaji mkubwa.”

“Hatuko tayari na hatutaki kukubali kushindwa katika mapambano yetu ya kudai haki ya matokeo ya uchaguzi. Tunataka kuona mshindi akitangazwa kwa vigezo,” amesema Kabwila.

Jumanne, wapiga kura milioni 7 walipiga kura kuchagua rais mpya, wabunge, na madiwani watakaoongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.

Wito wa utulivu

Chakwera, ambae anagombea kwa mara ya pili, na aliyekuwa rais wa nchi hiyo Arthur Peter Mutharika kutoka chama cha Democratic Progressive Party ndio waliochuana vikali katika uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ametaka kuwepo kwa hali ya utulivu na kuwatahadharisha wafuasi wa chama dhidi ya kuchochea vurugu na “kuweka shinikizo.”

Wanne kati ya wagombea urais 17 tayari wamekubali kushindwa kufuatia matokeo ya awali yanayoendelea kutoka.

CHANZO:AA