Kasi ya biashara yapungua jijini Dar es Salaam Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Jiji la kibiashara la Dar es Salaam nchini Tanzania linafahamika kama kitovu cha biashara nchini humo. Mbali na biashara mbalimbali zinazofanyika lakini bandari kuu ya nchi hiyo pia iko jijini Dar es Salaam.
Kasi ya biashara yapungua jijini Dar es Salaam Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Jiji la Dar es Salaam, Tanzania. / TRT Afrika
25 Oktoba 2025

Kutokana na sifa hiyo, jiji hilo limezoeleka kwa mishe mishe zake za kila siku. Hata hivyo, baadhi ya wakazi wake ambao ni wananchi wa kipato cha chini, hasa wachuuzi na wafanyabiashara ndogo ndogo wanakiri kwamba, katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, biashara imepungua.

Muhsin Seif, ni muuza mahindi ya kuchoma jijini humo katika eneo la Mnara wa Saa, "Ni kweli hali halisi kidogo kumepooza pooza kutokana na Uchaguzi, wengi wapo katika pirika pirika za Uchaguzi.

Nae Henry Magessa, anayejishughulisha na usafirishaji, anasema wanaendelea kufanya biashara lakini sio kama ilivyokuwa awali.

"Tunafanya biashara japo mzunguko sio mzuri kama zamani. Labda kwa sababu ya hizi kampeni labda zinaweza kuwa zimechangia kwa sababu wengi tuliokuwa tunawapa huduma hivi sasa hawapo."

Wakati huo huo, waandishi wa habari wa TRT Afrika, ambao wapo jijini humo kufuatilia matukio mbalimbali nchini humo, wamekiri kwamba, hali ya jiji kidogo imezizima, tofauti na siku za kawaida ambapo kunakuwa na msongamano mkubwa wa magari.

Hali hii inaweza kuwa inachangiwa na taarifa zinazoendelea kuenea mitandaoni za baadhi ya watu wakidai kuwepo kwa maandamano siku hiyo ya kupiga kura. Taarifa ambazo Rais Samia Suluhu Hassan wa nchi hiyo amesema kuwa maandamano pekee yatakayokuwepo siku hiyo ni ya kupiga kura.

Tayari Oktoba 29 ambapo itakuwa ni siku ya Jumatano imetangazwa kuwa siku ya mapumziko, kwa lengo la kuwapa fursa Watanzania kujitokeza kwa wingi ili kupiga kura. Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo, kuna takriban wapiga kura milioni 34 waliojiandikisha.

Kwa upande wake, Jeshi la Polisi nchini humo limewahakikishia raia kuwepo kwa ulinzi wa kutosha na vile vile kuwaonya wale watakaokuwa na malengo ya uvunjifu wa amani.

Lakini licha ya wasiwasi na hofu iliyotanda, shilingi ya Tanzania inaonekana kuzidi kuwa imara dhidi ya dola.


CHANZO:TRT Afrika