Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia raia wa nchi hiyo kuwa Uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 utafanyika kwa usalama, akisisitiza kuwa uchaguzi ni takwa la kidemokrasia na siyo vita.
Rais Samia ametoa kauli hiyo Septemba 17, 2025 wakati wa mkutano wake wa kampeni katika viwanja vya Kanjengwa, Jimbo la Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.
Mgombea huyo, ambaye alikuwa akishiriki mkutano wake wa kwanza wa kampeni kwa upande wa Zanzibar, alisema kuwa utulivu wa kisiasa ni nguzo muhimu ya maendeleo ya nchi.
“Ninawaomba sana twende tukadumishe amani. Uchaguzi si vita; uchaguzi nit endo la kidemokrasia, ni watu kwenda kupiga kura kwa utaratibu mlivyokubaliana,” alisema mgombea huyo.
Rais Samia, pia aliwataka watanzania kurejea majumbani mwao mara baaday kupiga kura, akiwasihi kuepuka vurugu ili nchi hiyo ibaki salama.
Kulingana na mgombea huyo, vyombo vya ulinzi na usalama viko tayari kuilinda nchi hiyo.