| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Mvua kali zasababisha mafuriko Gaza, na kuharibu maelfu ya mahema ya wakimbizi
Takriban watu 14 wamefariki dunia kutokana na dhoruba kali ya upepo na baridi Gaza.
Mvua kali zasababisha mafuriko Gaza, na kuharibu maelfu ya mahema ya wakimbizi
Mvua kubwa na upepo mkali umeharibu mahema ya wakimbizi Gaza. / AA
tokea masaa 18

Mvua kubwa zinazonyesha huko Gaza, zimesababisha mafuriko katika maelfu ya mahema yanayotumiwa na Wapalestina, huku maji yakiingia katika hospitali ya eneo hilo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Anadolu, maji ya mvua yaliingia sehemu za Hospitali ya Al-Shifa Gaza, hasa maeneo ya mapokezi na kitengo cha dharura, na kuathiri shughuli za hospitali.

Hospitali ya Al-Shifa, kituo kikubwa cha matibabu cha Gaza, imekumbwa na mashambulizi mengi ya Israeli katika kipindi cha miaka miwili ya mauaji ya halaiki na sehemu kubwa kuharibika.

Juhudi za Wizara ya Afya ya Gaza za kurudisha huduma baada ya kusitishwa kwa mapigano hazijafanikiwa kutokana na Israel kuzuia kuingia kwa vifaa vinavyohitajika.

Mashuhuda waliiambia Anadolu kwamba maelfu ya mahema ya watu waliokimbia makazi yameathiriwa na mafuriko na kuangushwa na upepo mkali uliokuwa unavuma katika eneo hilo tangu Jioni ya Jumatatu.

“Tuliamshwa na sauti ya upepo mkali uliogonga hema letu. Tulijaribu kulilinda na kulishikilia, lakini upepo uliangusha hema, na vitu vyetu vyote vilirushwa mbali,' Khaled Abdel Aziz, Mpalestina aliyekimbia makazi, aliiambia Anadolu.

Mamia ya Wapalestina walijaribu kupata hifadhi dhidi ya mvua chini ya majengo yaliyoharibiwa na jeshi la Israeli Ghaza, kwa mujibu wa mashuhuda.

Wakati huo huo, Mpalestina Maha Abu Jazar alikuwa akikimbia bila mwelekeo pamoja na watoto wake watatu baada ya maji kujaa katika hema lake lililopo mtaa wa Al-Mawasi, magharibi mwa Khan Younis, kusini mwa Gaza.

Msemaji wa ulinzi wa kiraia wa Gaza, Mahmoud Basal, aliwatahadharisha dhidi ya kujikinga chini ya nyumba zilizoharibiwa wakati wa mauaji ya halaiki ya Israeli kwamba ziko hatarini kuanguka wakati wowote kutokana na mvua na upepo mkali.

“Nyumba hizi zinatishia maisha ya mamia ya maelfu ya Wapalestina ambao hawajapata pa kukimbilia,' Basal aliiambia Anadolu. “Tumeonya dunia mara kadhaa, lakini bila mafanikio.”

Takriban watu 14 waliuawa wakati wa Kimbunga Byron Gaza wiki iliyopita. Zaidi ya mahema 27,000 za wakimbizi yaliathirika kwa kusombwa na maji au kuchanika kutokana na upepo mkali, na majengo 13 yalianguka kote Gaza.

Ingawa utekelezaji wa kusitishwa kwa mapigano ulianza Oktoba 10, hali ya maisha Gaza haijaboreshwa, kwani Israel inaendelea kuweka vikwazo vikali kwa kuzuia kuingia kwa magari ya misaada, ikikiuka itifaki ya kibinadamu ya makubaliano.

Israel imeua zaidi ya watu 70,600, wengi wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi zaidi ya 171,100 wengine katika mashambulizi ya tangu Oktoba 2023, ambayo yameendelea licha ya kusitishwa kwa mapigano.