| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Rais Putin wa Urusi ampongeza Rais Museveni wa Uganda
Rais Yoweri Museveni alipata asilimia 71.6 ya kura katika uchaguzi wa urais uliofanyika tarehe 15 Januari, na hivyo kushinda muhula wa saba madarakani.
Rais Putin wa Urusi ampongeza Rais Museveni wa Uganda
Rais Putin alipokutana na Rais Museveni mjini Sochi wakati wa Mkutano wa kilele wa Urusi na Afrika 2019. / / Reuters
tokea masaa 17

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amempongeza Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwa kushinda muhula wa saba.

Ushindi huo unaendeleza utawala wa Museveni wa zaidi ya miaka 40 nchini humo.

Katika barua aliyomwandikia Museveni tarehe 22 Januari, Rais Putin alimtakia kiongozi huyo wa Uganda “mafanikio, afya njema na ustawi.”

Putin pia alieleza matumaini yake kwamba kuchaguliwa tena kwa Museveni kutaimarisha ushirikiano kati ya Urusi na Uganda kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Urusi imekuwa taifa la kwanza kubwa lenye ushawishi wa kisiasa, kijeshi na kiuchumi duniani kumpongeza Museveni kufuatia uchaguzi wa wiki iliyopita.

Hapo awali, viongozi wengi wa Afrika wamempongeza kiongozi huyo wa Uganda mwenye umri wa miaka 81, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986.

Ushindi wa Rais Museveni, kama ulivyotangazwa na tume ya uchaguzi, umempa muhula wa saba wa miaka mitano.

Museveni aendelea kuiongoza Uganda

Museveni alipata asilimia 71.6 ya kura huku mpinzani wake mkuu Bobi Wine akipata asilimia 24.7.

Bobi Wine amekataa kukubali matokeo hayo, akidai kulikuwa na dosari na udanganyifu katika uchaguzi.

Upinzani pia umedai kuwa kulikuwa na vitendo vya vurugu dhidi ya wafuasi wa Bobi Wine.

Hata hivyo, mamlaka za serikali zimekanusha madai hayo na kusema kuwa wafuasi wa upinzani ndio waliosababisha vurugu wakati wa uchaguzi, na watu wengi walikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na ghasia.

Museveni, ambaye ni mmoja wa viongozi waliodumu madarakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika, anatarajiwa kuendelea kuongoza hadi mwaka 2031.

Ingawa wakosoaji wake wanamtuhumu kwa kutumia nguvu kupita kiasi, wafuasi wake wanamsifu kwa kudumisha amani na utulivu wa Uganda pamoja na kukuza uchumi.

Aidha, nchi hiyo inatarajiwa kuanza uzalishaji wa kibiashara wa mafuta ghafi baadaye mwaka huu.

CHANZO:TRT Afrika